Rubi ya Mundarara Longido yapaisha vipato vya wananchi

NA GODFREY NNKO

SAFARI ya kilomita 85 kutoka Arusha Mjini hadi Mundarara Ruby Mine imenikutanisha na wananchi wanaozunguka mgodi unaochimba madini ya Rubi uliopo katika Kijiji cha Mundarara katika Tarafa ya Engarenaibor Wilaya ya Longido mkoani Arusha.
Baadhi ya wananchi wakiendelea kuitafuta Rubi karibu na mgodi huo, katika soko la Dunia inatajwa kuwa na thamani kubwa katika kundi la madini ya vito.

Wakiwa na nyuzo za tabasamu huku wakiendelea na majukumu yao, wananchi hao wameupongeza mgodi huo kwa kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Sambamba na kuwashirikisha katika shughuli za uchimbaji madini ambazo zimekuwa mkombozi katika maisha yao na familia.

"Tunaishukuru sana Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuendelea kuvutia wawekezaji katika Sekta ya Madini, hapa Mudarara nasi watu wenye ulemavu tunakula, tunavaa na kukidhi mahitaji yetu kutokana na shughuli za mgodini.
"Mimi ni miongoni mwa watu wenye mahitaji maalumu, lakini sijawaza kwenda huko mjiji kuombaomba, kwani nikiwa na familia yangu tukipewa mfuko wa mawe tunashirikiana kuchambua na tunapata kipato kizuri,"amesema Naata Nangoli mkazi wa kijji hicho ambaye ana mahitaji maalumu.

Ameyasema hayo Machi 23,2024 ikiwa kwa nyakati tofauti wananchi wamewaeleza mambo mengi waandishi wa habari wanaofanya ziara ya kutembelea mgodi huo kwa lengo la kujionea shughuli za uchimbaji madini.
Naye Leita Molleli amesema kuwa, mgodi wa Mundarara umekuwa mkombozi katika maisha yao ambapo kupitia mgodi huo wananufaika na huduma mbalimbali.

Akitolea mfano baadhi ya huduma hizo ni pamoja na kupata ajira, kupata mchanga wa madini,ujenzi wa madarasa , uboreshaji wa makazi kupitia biashara ya madini wanayofanya mgodini hapo.
Kwa upande wake Meneja Madini katika Mgodi wa Mundarara Ruby Mine akitokea R-Gi Company Limited, Frank Michael Luholela amesema,R-Gi Company Limited ni mshirika wa STAMICO kwa upande wa Serikali.

Amesema, walianza kuwekeza katika mgodi huo mwaka 2021 wakiwa na makubaliano ya pande zote mbili kwa maana ya R-Gi Company Limited na STAMICO upande wa Serikali.

"Tangu tumeanza tumekuwa wadau wakubwa wa Serikali kwa maana ya kulipa kodi kwa kile ambacho tumekuwa tukikizalisha na mchango mzima katika jamii ikiwemo kutoa ajira."
Amesema, walipofika mara ya kwanza mgodini hapo aliyekuwa mbia wa kwanza aliwaachia wafanyakazi zaidi ya 200 ambao walikuwa wanadai mishahara.

"Ilikuwa mishahara ya muda mrefu, lakini sisi tulivyoingia tuliamua kuchukua kwanza lile jukumu ili tuweze kuendelea na tulifanikiwa hilo."

Meneja Madini huyo anasema, kwa sasa mgodi huo una jumla ya wafanyakazi 143.

"Mgodi wetu ni conversation underground mine, ikimaanisha tunafuata trends ya ile vein na product ambayo inazalishwa hapa ni rubi gems,rubi zoisite na light."
Amesema, mgodi huo mara ya kwanza ulikuwa umeenda umbali wa mita 500 lakini, yalitokea matatizo ya kimipaka hivyo baada ya ufumbuzi wakabakia na kina cha mita 320.

"Lakini, ukiachana na deep ya 320 tume-drive horizontal, tuna extension mpaka ya mita 500 kwa upande wa West na kwa upande wa East tunaishia mita 100."

Amesema, madini hayo ya vito yanatumika kwa ajili ya urembo.

"Katika madini ya vito, size inavyokuwa kubwa ndiyo product inakuwa na ubora zaidi ukiangalia muonekano, rangi ilivyokaa unapata ule uhalisia kwamba hii ni quality game."
Luholela amesema kuwa, mgodi unaendelea kutekeleza kanuni ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) hususani katika masuala yanayohusu maendeleo ya jamii.

Ameongeza kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu ya uchimbaji, mgodi umeendelea kutoa ushirikiano kwa wananchi wanaouzunguka kwa kuwapatia mifuko ya mawe ya madini yanayochimbwa katika mgodi ambapo huchambua na kupata madini ambayo wanauza na kupata kipato.

Kuhusu changamoto ya mgodi, Luholela ameeleza kuwa,kwa sasa changamoto kubwa na mipaka ya chini kwa sababu kunatokea mitobozano katika uchimbaji jambo linalopelekea kushindwa kuendelea na uchimbaji.
Historia inaonesha kuwa, uchimbaji rasmi wa madini ya rubi (ruby) katika Kijiji cha Mundarara ulianza mwaka 1948 ukifanywa na kampuni ya kigeni iliyokuwa imesajiliwa nchini Kenya iliyojulikana kwa jina la Continental Ore Company Ltd.

Aidha,baada ya Tanganyika kupata Uhuru mwaka 1961 Serikali ilichukua hatua ya kuutaifisha mgodi huo mwaka 1973 na kuukabidhi kwa Tanzania Gemstone Industries ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

Hata hivyo,Mundarara Ruby Mine kwa ushirikiano kati ya STAMICO na R-Gi Company Limited ulianza uchimbaji mwaka 2021.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news