Serikali kupitia SELF Microfinance Fund inavyowawezesha wananchi kuaga umaskini nchini

NA GODFREY NNKO

MFUKO wa SELF (SELF Microfinance Fund) nchini umesema,huwa unatoa mikopo kwa njia mbili ili kukuza sekta ya huduma ndogo za fedha kwa ajili ya kupunguza umaskini nchini.

Njia hizo ni mikopo kupitia taasisi ndogo za fedha ili kusaidia kupeleka huduma za kifedha kule ambako SELF haifiki na mikopo ya moja kwa moja kwa wanufaika.
Hayo yamesemwa leo Machi 11,2024 jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa mfuko huo,Mudith Cheyo katika kikao kazi na wahariri wakiwemo waandishi wa habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Pia, amesema mfuko huo huwa unatoa elimu ya fedha na kujengea uwezo taasisi ndogo za fedha.

"Elimu ya fedha utolewa kwa wateja wote. Wateja wa vikundi upewa mafunzo zaidi ya vikundi na taasisi za huduma ndogo za fedha upewa mafunzo ya kujengewa uwezo wa kuendesha taasisi zao."

Cheyo amesema, pia huwa wanatoa huduma ya uwakala wa bima ambapo wamekuwa wakihamasisha wananchi kujikinga na majanga kwa kukata bima.
Kwa upande wa mikopo, Cheyo amesema mfuko huo unatoa mikopo kwa taasisi ndogo za fedha-MFIs/SACCOS.

Mikopo hiyo inalenga wanufaika wanaofanya biashara au kilimo ambapo riba ya mikopo hii ni kati ya asilimia 16 hadi 18 kwa mwaka.

Amesema,mikopo ya moja kwa moja kwa wanufaika,walengwa wa mikopo hii ni wajasiriamali wadogo na wakati-MSMEs, wakulima wadogo na wafugaji.

Pia, huwa wanatoa mikopo kwa ajili ya kuboresha makazi, vikundi, kwa ajili ya nishati safi ya kupikia na mikopo kwa ajili ya watumishi wa umma huku riba ya mikopo hii ni kati ya asilimia 15 hadi 22.

Cheyo amesema, mfuko huo ni mkopeshaji wa jumla kwa taasisi ndogo za fedha ambapo huwa wanazikopesha na kuzijengea uwezo taasisi ndogo za fedha.

"Kwa sasa tunakopesha taasisi ndogo za fedha zaidi 200 nchi nzima."

Kuhusu SELF SM

SELF Microfinance Fund (SELF MF) ni taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Fedha inayoshughulika na utoaji wa mikopo hasa kwa wananchi wa kipato cha chini waweze kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali ili kujiongezea kipato na kupunguza umasikini.

Aidha, ulianza kutekeleza majukumu yake Julai Mosi, 2015, ukirithi majukumu ya Mradi wa Serikali uliojulikana kama Small Entrepreneurs Loan Facility (SELF Project) ambao ulitekelezwa kati ya mwaka 1999 hadi 2000 na mwaka 2014 hadi 2015.
Hata hivyo, licha ya mfuko huu kuwa chini ya Wizara ya Fedha pia ni miongoni mwa taasisi na mashirika ya umma ambayo yanasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

TR ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.

Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mnamo mwaka 2010 kulifanyika mabadiliko makubwa ya sheria ambapo moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa ofisi inayojitegemea kimuundo.
Afisa Habari na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akiongoza kikao hicho.

Vile vile, katika mwaka 2014 baada ya kufutwa kwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) ofisi ilikabidhiwa majukumu ya shirika hilo.

Kikao kazi cha leo ni mwendelezo wa Ofisi ya Msajili wa Hazina kuzikutanisha taasisi na mashirika hayo ya umma na wahariri ili ziweze kuelezea walikotoka, walipo na wanapoelekea.

Dhamira ikiwa ni ili umma ambao ndiyo wamiliki wa taasisi hizo waweze kupata mwelekeo wake na kufahamu mafanikio yao.

Afisa Mtendaji Mkuu huyo amefafanua kuwa, wanufaika wa mfuko huo wanatoka katika mikoa 30 ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani.

Vile vile amefafanua kuwa, mfuko huo unafanya kazi nchi nzima kupitia matawi 12 ambayo yanajumuisha Mkoa wa Dar es Salaam ambalo linahudumia mkoa huo wenyewe na Mkoa wa Pwani.

Tawi la pili, Cheyo amsema ni la Zanzibar ambalo linahudumia Unguja na Pemba huku tawi la Kahama likihudumia mikoa ya Shinyanga, Tabora na Katavi.
"Na tawi la Morogoro linahudumia mkoa huo ambapo lile la Arusha linahudumia mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro. Tawi la Geita linahudumia mikoa ya Geita na Kagera huku Mtwara lilikihudumia mikoa ya Mtwara na Lindi."

Kwa upande wa tawi la Mwanza linahudumia mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu ambapo lile la Iringa linahudumia Mkoa wa Iringa, Ruvuma na Njombe huku Tanga ikihudumia Mkoa wa Tanga. 

Aidha, tawi la Mbeya linahudumia mikoa ya Mbeya, Rukwa na Songwe. Huku lile la Dodoma likihudumia Dodoma yenyewe na Shinyanga.

Pia,amesema Mradi wa SELF ulikuwa ni miongoni mwa programu za Serikali zinazotekeleza jukumu la kupunguza umaskini kwa niaba ya Serikali ambayo ilifadhiliwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).
Amesema, mradi ulilenga katika kuongeza mchango wa biashara ndogo za kati, katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini na kuimarisha tasnia ya mikopo midogo midogo nchini Tanzania.

Ni kupitia Mfuko wa Mkopo wa Jumla kwa Taasisi Ndogo za Fedha zinazostahiki (MFIs), kuimarisha uwezo wa kushirikiana MFIs kupitia mafunzo na usaidizi wa kitaasisi na kukuza na kuhamasisha uundwaji wa MFIs mpya za msingi nchini.

Katika hatua nyingine, Afisa Mtendaji Mkuu huyo amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan, mfuko huo umepata faida ya shilingi bilioni mbili huku ukitoa gawio kwa Serikali zaidi ya shilingi milioni 240.

“Tumekuwa tukikua mwaka hadi mwaka, na tumepata faida ya shilingi bilioni mbili, tukatoa gawio la zaidi ya shilingi milioni 240, huku mtaji ukiongezeka kutoka shilingi bilioni 56 hadi 62,” amesema Cheyo.

Pia, amesema mikakati yao ni ifikapo mwaka 2026 mfuko uwe na matawi 20 kutoka 12 ya sasa, huku akisisitiza kuwa wamejipanga kuondoa mikopo kausha damu nchini.

Cheyo amesema,kupitia mkakati wa kuongeza matawi wanatarajia kwa siku za karibuni watalifikia kundi kubwa la Watanzania hasa kwenye SMEs ambao wanakadiriwa kufikia zaidi ya milioni nne.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news