Serikali yachukua hatua madhubuti kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa,tabianchi

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema, Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.
Amesema, wanafanya hivyo kwa sababu hali hizo zimeendelea kuathiri utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Miongoni mwa shughuli zinazoathirika ni pamoja na kilimo, ujenzi, utalii, miundombinu, usafirishaji, nishati na afya.
Mifano ya hivi karibuni ni mvua kubwa zilizochagizwa na uwepo wa El Nino na kusababisha vifo na uharibifu wa miundombinu hasa barabara na nyumba za watu.

Prof.Mbarawa ameyasema hayo leo Machi 23,2024 jijini Dodoma kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani.

"Hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukabiliana na janga hili la mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, ni pamoja na uboreshaji wa huduma za hali ya hewa.
"Na uimarishaji wa mfumo wa utoaji tahadhari (Early Warning Systems) nchini."

Amesema,uboreshaji huo pia ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ibara ya 59 J ikiweka malengo ya kuimarisha miundombinu na huduma za hali ya hewa nchini.

Prof.Mbarawa amesema, uboreshaji huo pia ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma za hali ya hewa ili kufika kwa jamii katika ngazi zote nchini (National Framework for Climate Services-NFCS).
"Ni kwa lengo hilo hilo la kukabiliana na kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na kuhakikisha usalama wa chakula na afya pamoja na matumizi bora ya vyanzo vya maji."

Katika kuboresha huduma za hali ya hewa na tahadhari za hali mbaya ya hewa nchini, Profesa Mbarawa amesema, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya hali ya hewa.

"Ikiwa ni pamoja na ununuzi na ufungaji wa mitambo ya kisasa ya upimaji na uchakataji wa taarifa za hali ya hewa, kompyuta kubwa ya kisasa na yenye uwezo mkubwa wa kuchakata data za hali ya hewa.
"Kompyuta hii inaiwezesha TMA kuboresha na kuongeza usahihi wa utabiri wa hali ya hewa hususani kwa maeneo madogomadogo, ambapo huduma hiyo imeshaanza kutolewa hadi ngazi ya wilaya kwa utabiri wa mvua za msimu."

Vile vile amesema, Serikali iko hatua za mwisho kukamilisha mtandao wa jumla ya rada saba za hali ya hewa, ambapo katika kipidi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita, malengo ya ununuzi wa rada nne yamefikiwa.

Amesema,kati ya hizo Rada mbili zinakamilishwa kufungwa katika mikoa ya Mbeya na Kigoma na utengenezaji wa rada nyingine mbili zitakazofungwa katika mikoa ya Kilimanjaro na Dodoma unaendelea kiwandani nchini Marekani.
Waziri Prof.Mbarawa amesema, rada hizo zinatarajiwa kukamilika na kufungwa mwaka huu wa 2024.

Pia, amesema Rada nyingine tatu zimekamilika na kufungwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Mtwara.

"Hatua hii inaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza Kikanda (Afrika Mashariki) kuwa na idadi kubwa ya rada za hali ya hewa na kuimairisha huduma za uangazi na utabiri wa matukio ya hali mbaya ya hewa."

Amesema,Serikali imetambua changamoto kubwa iliyopo kwa baadhi ya maeneo yanayoathirika na radi za mara kwa mara na imenunua seti tano za vifaa vya utambuzi wa matukio ya radi (lighting detectors).
Vifaa ambavyo amesema,vimefungwa katika maeneo ya Musoma, Mwanza, Kagera (Bukoba), Tabora na Kigoma (Kibondo).

Mbali na hayo, Waziri Mbarawa amesema,Siku ya Hali ya Hewa Duniani ni kumbukizi ya kuanza kutumika kwa Mkataba wa kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) tarehe 23 Machi 1950.

Hivyo, Siku ya Hali ya Hewa Duniani husherehekewa kila ifikapo tarehe 23 Machi ya kila mwaka kwa kuongozwa na ujumbe wa kaulimbiu.

Kaulimbiu ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka huu wa 2024 iliyopitishwa na nchi wanachama wa WMO, ni ”At the frontline of climate action” (Kuwa Mstari wa Mbele Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi).

TMA

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt.Ladislaus Chang’a amesema,maadhimisho haya huonesha mchango na umuhimu wa taasisi za Kitaifa zinazotoa huduma za hali ya hewa kwa usalama na ustawi wa jami.
Dkt.Chang'a ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) amesema;

"Tanzania ikiwa ni miongoni mwa Nchi 193 wanachama wa WMO inaungana na Jumuiya ya Kimataifa kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani na kuonesha dhamira yake ya kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi."

Amesema,kaulimbiu ya mwaka huu ilichaguliwa kwa kuzingatia lengo la 13 la Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goal 13-Climate Action).

Lengo ambalo linaitaka jamii kuchukua hatua za haraka kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
"Mpaka sasa, mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi yameathiri kila nchi katika kila bara na pia tunatambua kuwa ripoti za Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) zinaangazia kuwa kumekuwepo na ongezeko kubwa la joto ambalo halijawahi kushuhudiwa sambamba na kuongezeka zaidi kwa matukio ya hali mbaya ya hewa na athari zake.

"Athari hizi zinazidi kuongezeka na kusababisha changamoto mbalimbali katika uchumi wa taifa na kuathiri maisha ya kila siku na hata ya baadae."

Aidha, amesema kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi chafuzi kunakotokana na shughuli za viwanda kumesababisha wastani wa joto duniani kupanda zaidi ya nyuzi joto moja (1°C) ikilinganishwa na viwango vya mwaka 1850 - 1900.
Kwa upande mwingine, Dkt.Chang'a amesema, mwaka 2023 ulivunja rekodi kwa kuwa mwaka wenye joto zaidi katika historia ya dunia ukichagizwa na ongezeko la gesijoto na uwepo wa hali ya El Niño.

"Wastani wa ongezeko la joto kidunia kwa mwaka 2023 ulkuwa nyuzi joto 1.4 °C ikilinganisha na kipindi cha kabla ya mapinduzi ya viwanda.

"Kwa upande wa Tanzania ongezeko la joto kwa mwaka 2023 lilifikia nyuzi joto 1.0 0C. Ongezeko hili kubwa likiambatana na matukio ya hali mbaya ya hewa, ikiwemo mvua kubwa, mafuriko na upepo mkali vimechangia kuleta maafa ikiwemo vifo na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu."

Kwa muktadha huo, amesema WMO na wanachama wake wanaweka vipaumbele vya kuimarisha huduma za hali ya hewa sanjali na kuelimisha jamii kuhusu matumizi stahiki ya huduma na taarifa za hali ya hewa.
"Huduma za hali ya hewa zinazotolewa nchini Tanzania zimeendelea kuwa bora zaidi katika historia ya nchi yetu kabla na baada ya uhuru.

"Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa katika ununuzi na uboreshaji wa miundombinu ya uangazi sambamba na wafanyakazi kujengewa uwezo."

Amesema,maboresho hayo ni pamoja na ufungaji wa vifaa vya kisasa vya kuhakiki utendaji kazi wa vifaa vya hali ya hewa (Calibration Laboratory Equipments), rada za hali ya hewa.

Pia,vifaa vya utambuzi wa matukio ya radi (Lightning detector) na kompyuta yenye uwezo mkubwa wa kuchakata data za hali ya hewa (Computer cluster).

"Uwekezaji huu umeongeza kwa kiasi kikubwa ubora na usahihi wa taarifa za utabiri wa hali ya hewa na tahadhari za mapema hadi kufikia wastani kati ya asilimia 80 hadi 98 juu ya asilimia 70 inayokubalika kimataifa.

"Hii inazifanya huduma za TMA nchini kuwa za uhakika na kuchangia kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi sambamba na kuokoa maisha na mali kutokana na matukio ya hali mbaya ya hewa."
Amesema,TMA inaendelea kuwa mstari wa mbele kutoa mchango katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kwa kutfanya tafiti na kuhamasisha matumizi ya sayansi.

Sambamba na uvumbuzi miongoni mwa wataalamu wake na wataalamu wengine katika vyuo vikuu na taasisi za utafiti nchini na barani Afrika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news