Uchumi wa Tanzania waendelea kukua huku TRA ikirekodi mafanikio makubwa

NA GODFREY NNKO

SERIKALI imesema, uchumi wa Tanzania umeendelea kkukua hadi kufikia asilimia 5.2 licha ya athari kubwa za mlipuko wa UVIKO-19 duniani pamoja na vita kati ya Urusi na Ukraine.
Msemaji Mkuu wa Serikali,Mobhare Matinyi ameyasema hayo leo Machi 24,2024 jijijni Dar es Salaam wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan madarani.

Amesema, matatizo hayo yaliutikisa uchumi wa Tanzania ambao uliokuwa umefikia wastani wa ukuaji wa zaidi ya asilimia 7 na kuushusha hadi asilimia 4.2 mwaka 2020.

Licha ya hayo Matinyi amesema kuwa, kwa sasa ukuaji umefikia asilimia 5.2 kutokana na uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita.

“Aidha, Tanzania imeendelea kuwa katika kundi la nchi zenye uchumi wa pato la kati, ikimaanisha pato la wastani la kila mwananchi kwa mwaka ambapo ingawa mwaka 2019 ilikuwa kiasi cha dola 1,080, lakini mwaka 2022 ni dola 1,200.

“Serikali pia imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei ambapo kwa sasa ni chini ya asilimia 4- kiwango ambacho ni miongoni mwa viwango bora katika nchi za jumuiya za kikanda ambazo Tanzania ni mwanachama, kama Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)."

Katika hatua nyingine amesema, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa toshelezi ambapo katika kipindi chote cha miaka mitatu hadi Desemba 2023, nchi ilikuwa na akiba inayotosha kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi kwa miezi 4.5 ikiwa ni kiwango cha juu ya lengo la miezi 4.

"Akiba hiyo ni sawa na dola za Marekani bilioni 5.4,” amesema Matinyi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo.

Wakati huo huo, Matinyi amesema kuwa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kufanya vizuri katika kipindi cha miaka mitatu.

Ni kwa kufuata mwongozo wa Rais wa kujenga uhusiano mzuri na wafanyabiashara na kujali changamoto wakati wa kukusanya kodi nchini.

Amesema,makusanyo yamefikia shilingi trilioni 24.14 kwa mwaka 2022/23 kutoka shilingi trilioni 18.15 mwaka 2020/21 ikiwa ni ongezeko la shilingi trilioni 5.99.

“Aidha, kwa mwezi Desemba 2023, TRA ilivunja rekodi ya ukusanyaji ya kila mwezi baada ya kufanikiwa kukusanya shilingi trilioni 3.05 licha ya kuwa wastani kwa mwaka huu hadi sasa ni shilingi trilioni 2.13.

"Ni vema kufahamu kwamba hadi kufikia Machi 20, 2024, TRA ilikuwa imeshakusanya kiasi cha shilingi trilioni 19.21, ikiwa ni dalili mkwamba itavuka kiasi cha mwaka uliopita,” amesema Msemaji Mkuu huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news