Uingereza yazipa bidhaa za Tanzania kipaumbele cha kwanza kupitia DCTS

NA GODFREY NNKO

BALOZI wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar amewahakikishia Watanzania kuwa, kupitia mpango wake mpya wa kufanya biashara na nchi zinazoendelea wa UK-Developing Countries Trading Scheme-DCTS,bidhaa za Tanzania ndiyo kipaumbele cha kwanza katika soko lao.
“Ninaimani kubwa sana kwamba kwa pamoja tutaweza kufikia ongezeko kubwa la biashara kati ya Tanzania na Uingereza;

Balozi Concar ameyasema hayo leo Machi 28, 2024 jijini Dar es Salaam katika semina ya fursa za biashara na nchi ya Uingereza kupitia Mpango wa DCTS. Watanzania wengi wameshiriki semina hiyo moja kwa moja ukumbini huku wengine wakishiriki kwa njia ya mtandao ambapo wamepatiwa taarifa za muhimu kuhusu fursa ya kuuza bidhaa katika soko la Uingereza.

“Ninafikiri kwamba sasa ni wakati wa kufanya hivyo, kwanza tuna programu nzuri sana ya DCTS pili tuna utafiti mzuri sana kuhusu wafanyabiashara wa Tanzania.Kwa hiyo, Tanzania ndiyo ina bidhaa ambazo Uingereza inataka kununua,hivyo tufanye hivyo.”
Kupitia DCTS, Tanzania inatarajiwa kufanya biashara na Uingereza kupitia utaratibu ambapo inaweza kuuza nchini Uingereza asilimia 99.8 ya bidhaa zinazozalishwa nchini isipokuwa silaha bila kulipa ushuru.

Vile vile,asilimia 0.2 ya bidhaa zitaweza kuuzwa nchini Uingereza kwa kutozwa ushuru wa forodha kwa viwango vya asilimia 0 hadi 5.

Iwapo, Watanzanania watautumia vizuri mpango huo, mauzo ya Tanzania kwenda nchini Uingereza yataongezeka na kuchochea uzalishaji zaidi na hatimaye kuongezeka kwa mapato ya Serikali, fedha za kigeni na ajira kwa watu wengi.
Awali akifungua semina hiyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt.Ashatu Kijaji amesema,DCTS ni mpango mpya ambao umeanzishwa na Uingereza baada ya kujitoa rasmi katika Umoja wa Ulaya.

“Mpango huu umeanza kutumika rasmi Juni 19, 2023. Mpango huu wa biashara wa Uingereza na nchi zinazoendelea, kwa Tanzania umekuja katika muda muafaka, ambapo nchi yetu inafanya jitihada kubwa kurekebisha na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na miundombinu ili kupunguza gharama za ufanyaji biashara nchini.”

Waziri Dkt.Kijaji amesema kuwa, tangu mwaka 2016 biashara baina ya Tanzania na Uingereza imekuwa ikiegemea upande wa Uingereza ambapo tumekuwa tukinunua zaidi ya tunavyouza na kupelekea urari wa biashara kuwa hasi.
“Kwa mfano mwaka 2022 mauzo ya Tanzania kwenda Uingereza yalikuwa na thamani ya Shilingi za Tanzania bilioni 44 ikilinganishwa na manunuzi ambayo yalikuwa na thamani ya Shilingi za Tanzania tirioni 3.08 mwaka 2023.”

Amesema, mauzo yetu nchini Uingereza yalikuwa na thamani ya Shilingi za Tanzania bilioni 46 na manunuzi yalikuwa na thamani ya Shilingi za Tanzania tirioni 4.24.

Pia, kwa upande wa uwekezaji, taarifa kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonesha kuwa, kuanzia mwaka 1997 hadi Februari, 2024, jumla ya miradi 980 ya Kampuni za Uingereza yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 5,655.38 iliyotoa wastani wa ajira 126,322 katika sekta mbalimbali imewekezwa hapa nchini.

“Sekta zinazoongoza kwa uwekezaji huo ni uzalishaji viwandani iliyo na miradi 335 yenye thamani Dola za Marekani Milioni 835.11 na kuajiri Watanzania 43,728 ikifuatiwa na Sekta ya Utalii iliyo na miradi 227 yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 376.6 na ajira 15,199.”
Waziri Dkt.Kijaji amesema, takwimu hizo za biashara na uwekezaji bado ni ndogo ikilinganishwa na fursa ambazo nchi yetu inazo hususan katika bidhaa za mazao ya chakula.

Amreyataja mazao hayo kuwa ni matunda, mbogamboga, mazao ya mifugo, asali, madini na mazao mengine ya maliasili ikiwemo ya bahari na maziwa.

“Hivyo, ni matumaini yangu kuwa, mpango wa mpya wa Uingereza utasaidia katika kuimarisha na kukuza mauzo yetu kwenda Uingereza.”

Miongoni mwa faida za mpango huo mpya ni kupungua kwa kiasi kikubwa kwa masharti ya Uasilia wa Bidhaa (Rules of Origin) ambapo kutatoa nafasi kwa Tanzania kuweza kuagiza malighafi za kuzalisha bidhaa kutoka maeneo mbalimbali duniani na kuyaongezea thamani na kisha kuuza katika soko la Uingereza pasipo ushuru au kwa ushuru nafuu.

Pia,kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la Uingereza kutokana na kupungua kwa gharama za kufanya biashara kupitia kuondolewa kwa ushuru wa bidhaa.
Waziri Dkt.Kijaji ametaja faida nyingine kuwa ni urahisi wa upatikanaji wa taarifa kuhusu masoko na biashara nchini Uingereza na hivyo kutoa fursa kwa watanzania kuzichangamkia.

Sambamba na fursa ya makapuni ya Uingereza kushirikiana na makampuni ya nchini Tanzania kuwekeza na kuzalisha bidhaa bora zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news