Wekeza kwa mwanamke

NA LWAGA MWAMBANDE

KUELEKEA Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 8. Mwaka huu, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kujivunia michango ya wanawake katika taasisi mbalimbali za umma na katika jamii.
Ni kutokana na namna ambavyo wamekuwa wakiwajibika kikamilifu na kuwezesha matokeo chanya ambayo yamewezesha ustawi bora wa Taifa na jamii kwa ujumla.

Mwaka huu,ikiongozwa na kauli mbiu ya "Wekeza kwa Wanawake kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii"

Siku ya Wanawake Duniani ilianzia katika harakati za wafanyakazi na ikawa tukio la kila mwaka linalotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Aidha, mbegu za siku hii zilipandwa mwaka 1908, wakati wanawake 15,000 walipoandamana katika jiji la New York nchini Marekani wakidai muda mfupi wa kazi, mishahara bora na haki ya kupiga kura.

Mwaka mmoja baadaye, Chama cha Kisoshalisti cha Marekani kilitangaza Siku ya Kitaifa ya Wanawake ya kwanza. Wazo la kuifanya siku hii kuwa ya kimataifa lilitoka kwa mwanamke anayeitwa Clara Zetkin, mwanaharakati wa kikomunisti na mtetezi wa haki za wanawake.

Zetkin, alipendekeza wazo hilo mnamo 1910 kwenye mkutano wa kimataifa wa wanawake wanaofanya kazi huko Copenhagen. Wanawake 100 waliokuwepo, kutoka nchi 17 walikubali kwa kauli moja pendekezo lake.

Hata hivyo, tangu wakati huo hadi leo, siku hii imekuwa ya kusherehekea jinsi wanawake walivyofikia katika jamii, siasa na uchumi.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, ukiweza kwa mwanamke kamwe hautajutia maamuzi yako. Endelea;

1.Wekeza kwa mwanamke, ndiyo habari mjini,
Ninasema isikike, umuhimu kama dini,
Akikua mwanamke, mjini na kijijini,
Hayo ni maendeleo, kwa taifa na jamii.

2.Wekeza kwa mwanamke, umewekeza nyumbani,
Mama huyu mwanamke, anatuweka mjini,
Afanya tuongezeke, idadi hata thamani,
Hayo ni maendeleo, kwa taifa na jamii.

3.Wekeza kwa mwanamke, elimu ya darasani,
Ufanye aelimike, ujinga upigwe chini,
Akilini aamke, ashinde umasikini,
Hayo ni maendeleo, kwa taifa na jamii.

4.Wekeza kwa mwanamke, hata elimu ya dini,
Ili wana waleleke, kwa maadili ya dini,
Hekima waongezeke, wawe bora duniani,
Hayo ni maendeleo, kwa taifa na jamii.

5.Wekeza kwa mwanamke, kazi za maofisini,
Naye nafasi ashike, binafsi serikalini,
Kitaifa atumike, na hata ulimwenguni
Hayo ni maendeleo, kwa taifa na jamii.

6.Wekeza kwa mwanamke, apate shule chuoni,
Ifanye aongezeke, kuishi vema nyumbani,
Na magonjwa yapunguke, jinsi ala vitamin,
Hayo ni maendeleo, kwa taifa na jamii.

7.Wekeza kwa mwanamke, mikopo na isheheni,
Mwenyewe achakarike, jembe mifugo madini,
Mali na ziongezeke, twende juu toka chini,
Hayo ni maendeleo, kwa taifa na jamii.

8.Wekeza kwa mwanamke, kwa kweli yuko makini,
Mpe mkopo ashike, halafu ende kazini,
Marejesho na yafike, asiingie mitini,
Hayo ni maendeleo, kwa taifa na jamii.

9.Wekeza kwa mwanamke, ili tuwe kivulini,
Jasho huko litutoke, kisha turudi nyumbani,
Huko vema tutunzike, kesho tuende kazini,
Hayo ni maendeleo, kwa taifa na jamii.

10.Wekeza kwa mwanamke, hicho kipimo makini,
Kokote tukubalike, kwamba tuko duniani,
Usawa na usomeke, mlangoni dirishani,
Hayo ni maendeleo, kwa taifa na jamii.

11.Siku yake mwanamke, yatukumbusha kichwani,
Kwamba sote tuamke, yeye ashike mpini,
Kuzuri atupeleke, tuongezeke thamani,
Hayo ni maendeleo, kwa taifa na jamii.

12.Wekeza kwa mwanamke, Samia haumuoni?
Rais ni mwanamke, jinsi alivyo kazini,
Anafanya tuinuke, kwenda juu toka chini,
Hayo ni maendeleo, kwa taifa na jamii.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news