Amana za wateja Benki ya TCB zafikia shilingi trilioni 1.1, yaanika mafanikio

NA GODFREY NNKO

AFISA Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB),Adam Charles Mihayo amesema, amana za wateja wa benki hiyo zimeongezeka kwa asilimia 12 kufikia shilingi trilioni 1.1 za kitanzania.
Mihayo ameyasema leo Aprili 9, 2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri wakiwemo waandishi wa habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Amesema, hatua hiyo ni ishara kwamba, wateja wao wana imani kubwa na benki hiyo ambayo inatarajiwa kuadhimisha miaka 100 mwaka ujao.

"Pia,mikopo kwa wateja imepanda kwa asilimia 15.4 kufikia shilingi bilioni 983.6 za kitanzania hadi Machi 31, 2024. Hii inaonyesha dhamira ya benki katika kuwezesha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu wake."

Wakati huo huo, Mihayo amesema katika robo ya kwanza ya mwaka ambayo imefikia tamati Machi 31, mwaka huu wana ongezeko la faida ya shilingi bilioni 10.7 baada ya makato ya kodi.

"Benki inaamini ongezeko hili la asilimia 358 katika mapato yake kipindi cha robo ya kwanza yametokana na ukuaji mkubwa wa mapato katika aina zake zote za biashara na ongezeko kubwa la kitabu cha mizania katika kipindi tajwa kilichopitiwa.
"Mapato yaliongezeka kwa asilimia 30 mpaka kufikia shilingi bilioni 56.8 za kitanzania yakiimarishwa na kitabu cha mizania na kasi kubwa ya ukuaji katika mapato yote."

Amefafanua kuwa, ukuaji huo mkubwa unasukumwa na dhamira yao ya dhati na kujizatiti kwao katika ufanisi ili kumridhisha mteja.

"Sisi ni benki ambayo inachukua muda wake kuwasikiliza wateja wetu na kuweka juhudi katika kuelewa mahitaji yao,kwa ongezeko hili la mapato kwa asilimia 30 tumedhihirisha kwa mara nyingine tena ujasiri wetu, na uwezo wetu wa kulikabili soko linalokua kwa kasi.

"Imani ya wateja wetu kwetu bado ni imara kama inavyothibitishwa na ongezeko la amana ya wateja. Vile vile, dhamira yetu katika kuimarisha ukuaji wa uchumi inadhihirika wazi katika ongezeko la mikopo kwa wateja wetu.

"Tukiendelea na safari hii ya mafanikio, tunajizatiti kuwafikishia watu ubunifu wa kifedha na kuchangia katika ustawi wa watu wetu na Taifa letu kwa ujumla.”
Mihayo amesema, jumla ya gharama kulingana na kipato katika robo hiyo ya kwanza ni shilingi bilioni 43.2 za kitanzania, sawa na ongezeko la asilimia 6.1 ukilinganisha shilingi bilioni 40.7 za robo ya kwanza ya mwaka 2023.

Vile vile,amesema jumla ya gharama za uendeshaji imepanda kidogo kutoka shilingi bilioni 26.5 za kitanzania mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 2023 hadi kufikia shilingi bilioni 26.8 za kitanzania mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 2024.

"Tumejizatiti kuendeleza jitihada katika kutekeleza mkakati wetu ambao unazingatia ufanisi wa uendeshaji, na kuendelea kupunguza gharama zetu kwa uwiano wa mapato licha ya kuongezeka kwa kipindi hiki."

Amesema,benki hiyo inahusisha ukuaji huo wa faida na maendeleo endelevu ya biashara ndogondogo na za kati nchini.

Katika hatua nyingine, Mihayo amefafanua kuwa,katika kufikia lengo la benki juu ya wafanyabiashara wadogowadogo na wakati,wametumia njia ya kidigitali katika kufanya ufumbuzi wa kibenki, na hivyo kuwapa wateja wake ufanisi, urahisi na uwezo wa kufanya shughuli za kimiamala.

"Mwelekeo huu wa kimkakati unaimarishwa na mkakati wa kidigitali unaoendelea, ambao umeiwezesha benki kuwa karibu zaidi na wateja wake kuliko awali na kuwaruhusu wao kuendelea kujipatia huduma za kibenki katika sehemu zinazowapendeza wao na kuimarisha uhusiano wa kuaminiana kati ya benki na wateja wake."

Afisa Mtendaji Mkuu huyo amefafanua kuwa, pia mtandao wa mawakala wa kibenki wa TCB umekua kwa takribani mara nne katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Ni kutoka idadi ya mawakala 1,584 mwaka 2020 hadi zaidi ya mawakala 6,000 kwa mwaka 2023. "Idadi ya mashine za UmojaSwitch za ATM zimeongezeka kutoka 250 mwaka 2020 hadi kufikia mashine 281 kwa mwaka 2023.

"Katika kipindi hiki, TCB Benki pia imeanza kutoa kadi za VISA. UmojaSwitch imeingia ubia na NMB Benki na katika robo hii ya kwanza ya mwaka 2024, tayari kuna mashine za ATM 750 za NMB ambazo zimeunganishwa na ATM za UmojaSwitch.
"Hii inafanya jumla ya mashine za ATM za UmojaSwitch kufikia 1,031 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024. TCB Benki imeweza kuanzisha bidhaa bora kama vile, M-Koba.

"Ni matumaini ya uongozi kwamba tutaendelea kutoa bidhaa zinazowalenga wateja ambazo zitaendelea kuvunja rekodi kwa kipindi chote cha mwaka 2024 na kuendelea,"amefafanua Mihayo.

Kuhusu TCB

TCB ni zao la Tanganyika Postal Office Savings Bank (TPOSB) ambayo ilianzishwa mwaka 1925 wakati ambapo Tanganyika ilikuwa chini ya utawala wa Uingereza.

Mihayo amesema, TCB imepitia katika hatua mbalimbali ambapo baadaye ilikuwa Benki ya Akiba chini ya lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika ya Mashariki (EAP&TC) na ilikoma kufanya kazi baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aidha, Shirika la Posta na Simu Tanzania (TP&TC) lilianzishwa ili kuhudumia soko la Tanzania.

Afisa, Mtendaji Mkuu huyo amesema, TPB iliundwa kutoka kwa TP&TC ambapo ilianzishwa kwa Sheria ya Benki ya Posta Tanzania Na. 11 ya mwaka 1991.

Juni 29, 2015, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliifuta sheria hiyo na Machi 29, 2016 benki hiyo iliunganishwa chini ya Sheria ya Makampuni ( Sura ya 212) kama TPB Bank PLC.

Januari 19, 2017, benki ilizindua jina la TPB Bank PLC kwa umma pamoja na nembo yake mpya na Julai 14, 2021 benki ilibadilisha jina na kuwa Tanzania Commercial Bank Plc.

TCB inamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hisa asilimia 83.44, Shirika la Posta hisa asilimia 7.61, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hisa asilimia 2.91.

Wengine ni Posta na Simu Savings and Credit Cooperative Society Limited hisa asilimia 2.67,Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF hisa asilimia 2.35 na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) hisa asilimia 1.02.

Aidha,Benki ya TCB ni miongoni mwa taasisi na mashirika ambayo yapo chini ya Msajili wa Hazina nchini.

TR

Afisa Habari Mwandamizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akiongoza kikao hicho amesema, lengo la vikao hivyo ni kuondoa ukuta au pazia ambalo wengi walihisi taasisi hizo za umma zimejifungia ndani na zinafanya mambo yake kimya kimya.
"Na hata changamoto zinapotokea na ikatolea umma umepewa hizo taarifa mapokeo yake ni tofauti," amesema Sabato huku akifafanua kuwa,
Baada ya vikao kazi hivi ambavyo vimewapa Watanzania mwanga wa kile kinachoendelea ndani ya taasisi na mashirika ya umma, wamekuwa na uelewa mpana na hata taarifa zinapotoka wanakuwa hawana maswali mengi.

"Kwa hiyo tunaamini kwamba, kitendo cha kufanya hii mikutano inakutanisha umma pamoja na hizi taasisi tukiamini kwamba jukwaa hili au kundi hili la wanahabari lina nguvu ya kufikisha ujumbe kuhusu hizi taasisi."

Katika hatua nyingine, Ofisi ya Msajili wa Hazina imewapongeza wanahabari kwa kuendelea kuwa na mchango chanya katika kufikisha elimu kwa umma kuhusu yale yanayofanywa na taasisi na mashirika mbalimbali ya umma nchini.

Amesema, vikao hivyo vinatoa fursa kwa taasisi na mashirika ya umma kueleza yalipotoka, yalipo, yanapoelekea na mafanikio yake kwa ujumla.

Kuhusu TR

TR ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.

Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mnamo mwaka 2010 kulifanyika mabadiliko makubwa ya sheria ambapo moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa ofisi inayojitegemea kimuundo.
Vile vile, katika mwaka 2014 baada ya kufutwa kwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) ofisi ilikabidhiwa majukumu ya shirika hilo.

Kikao kazi cha leo na TCB ni mwendelezo wa Ofisi ya Msajili wa Hazina kuzikutanisha taasisi na mashirika hayo ya umma na wahariri ili ziweze kuelezea walikotoka, walipo na wanapoelekea.

Dhamira ikiwa ni ili umma ambao ndiyo wamiliki wa taasisi hizo waweze kupata mwelekeo wake na kufahamu mafanikio yao.

TEF

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatius Balile, Mjumbe wa Kamati Tendaji wa jukwaa hilo, Nevile Meena amesema, vikao kazi hivi ni daraja muhimu la kuwezesha umma kupata taarifa sahihi kutoka kwa taasisi na mashirika yao kupitia vyombo vya habari.

Pia, ameiomba TCB kuangalia uwezekano wa kuendelea kutoa elimu kwa waandishi wa habari hasa za biashara za Kiswahili ili kuweza kufikisha ujumbe sahihi kwa jamii juu ya nini kinafanyika ndani ya taasisi hiyo na faida zake nchini.
Meena amesema,habari za biashara mara nyingi zinagusa watu wengi ambao wanafahamu Kiingereza.

"Hivyo, ninaomba niwasilishe ombi kwenu kuelekea miaka 100 ya benki hii, ifikirieni sekta ya habari kwa maana ya waandishi wa habari za biashara ambao wataweza kuandika vizuri habari za Kiswahili zinazosomeka na kueleweka kwa wasomaji wa kawaida.

"Watu wakajua hapa TCB,kuna huduma ya mikopo kwa kusoma na kuelewa,"amefafanua Meena.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news