DCEA yafichua mbinu wanayotumia wafanyabiashara kusafirisha dawa za kulevya

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imesema,wafanyabiashara wa dawa za kulevya wamebuni mbinu mpya ya ufichaji wa dawa hizo ili waweze kuzisafirisha kwa kuzihusisha na bidhaa nyingine mbalimbali.
Picha zikionesha sehemu ya jumla ya kilogramu 353.52 za dawa za kulevya zilizokamatwa Kata ya Kunduchi jijini Dar es Salaam na watuhumiwa pembeni.

Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo, Aretas Lyimo ameyasema hayo leo Aprili 22,2024 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Ameeleza kuwa, baadhi ya dawa zilizokamatwa kupitia operesheni iliyofanyika Aprili 4 hadi 18,mwaka huu Mkoa wa Dar es Salaam, Tanga na Pwani zilikuwa zimefichwa kwa ustadi kwenye vifungashio vilivyoandikwa majina ya kahawa na chai ili kukwepa kukamatwa.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema, katika operesheni hiyo wamefanikiwa kukamata jumla ya kilo 767.2 za dawa za kulevya katika mikoa hiyo.
Dawa za kulevya zilizokamatwa eneo la Zinga Bagamoyo mkoani Pwani zikiwa kwenye viroba.
Kilo 1.49 ya dawa za kulevya aina ya skanka zilizokamatwa eneo la Wailes Temeke jijini Dar es Salaam.

Aina ya dawa zilizokamatwa ni pamoja na heroin kilo 233.2, methamphetamini kilo 525.67 na skanka kilo 8.33 wakiwemo watuhumiwa 21.

"Watuhumiwa 21 wamekamatwa kuhusiana na dawa za kulevya zilizokamatwa, baadhi yao wamefikishwa mahakamani na wengine watafikishwa taratibu za kisheria zitakapokamilika,"amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Amezitaja operesheni zilizofanikisha ukamataji wa dawa hizo kuwa ni ilizofanyika jijini Tanga eneo la Mikanjuni tarehe 4 Aprili,2024 ambapo watuhumiwa wawili walikamatwa na gramu 329.412 za heroin.
Gramu 329.412 za heroin zilizokamatwa Tanga.
Picha ikionesha sehemu ya jumla ya kilogramu 353.52 za dawa za kulevya zilizokamatwa Kata ya Kunduchi jijini Dar es Salaam.

Pia,operesheni iliyofanyika eneo la Wailes Temeke mtaa wa Jeshini jijini Dar es Salaam tarehe 8 Aprili, 2024 na kufanikisha watuhumiwa wawili kukamatwa na kilogramu 1.49 za skanka.

Nyingine ni iliyofanyika eneo la Zinga Bagamoyo mkoani Pwani tarehe 10 Aprili, 2024 na kufanikisha kuwakamata watuhumiwa watatu wakiwa na kilogramu 424.84 za dawa ya kulevya aina ya Methamphetamine.

Sambamba na mtuhumiwa mwingine mmoja alikamatwa na gramu 158.24 za heroin eneo la Kunduchi jijini Dar es Salaam tarehe 10 Aprili,mwaka huu.

"Aidha, tarehe 14 Aprili, 2024 tulifanya operesheni katika eneo la bandari jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kukamata kilogramu 4.72 za dawa za kulevya aina ya skanka pamoja na kuwakamata watuhumiwa watatu kuhusika na dawa hizo.
Nyumba zilipokamatwa kilo 424.84 za dawa za kulevya aina ya Methamphetamine eneo la Zinga wilayani Bagamoyo.
Magunia ya dawa za kulevya yaliyokamatwa na DCEA yakiwa yaefichwa chooni eneo la zinga Bagamoyo mkoani Pwani.

"Vilevile, tarehe 16 Aprili, 2024 tuliendelea na operesheni jijini Dar es Salaam, katika Kata ya Kunduchi na kukamata kilogramu 232.69 za dawa za kulevya aina ya heroin na kilogramu 100.83 za dawa ya kulevya aina ya methamphetamine zilizokuwa zinaingizwa nchini kupitia Bahari ya Hindi.

"Watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo ni tisa," amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Ameendelea kusema kuwa, mtuhumiwa mmoja alikamatwa tarehe 18 Aprili eneo la bandari jijini Dar es Salaam akiwa na kilogramu 2.12 za skanka.

Kamishna Jenerali Lyimo akiangazia tishio la dawa za kulevya linalokua kwa kasi duniani, ametoa wito kwa jamii kuungana katika kupambana na janga la dawa za kulevya kwani vijana ni kundi linaloathirika zaidi.
Picha mbalimbali zinazoonesha jumla ya kilogramu 353.52 za dawa za kulevya zilizokamatwa Kata ya Kunduchi jijini Dar es Salaam.

"Vijana ni nguvu kazi ya Taifa letu. Kama wakiendelea kuathiriwa na dawa za kulevya, uchumi na usalama wa nchi vitakuwa hatarini.

"Ni wajibu wa kila mmoja wetu kupambana na janga hili. Tunawaomba wananchi waendelee kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ili kulinda taifa letu dhidi ya janga hili kwa kupiga namba yetu ya bure 119,” amesema Lyimo.

Kamishna Jenerali Lyimo ametoa shukrani kwa wadau wote wanaoshirikiana na DCEA katika vita dhidi ya dawa za kulevya, hasa vyombo vya ulinzi na usalama na kuahidi kuwa DCEA itaendelea kupambana ili kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi salama na isiyo na dawa za kulevya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news