Serikali yaendeleza mapambano dhidi ya Malaria

DODOMA-Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu,Dkt. Jim Yonazi amesema, Serikali inaendelea na mipango yake ya kupanga mikakati ya namna ya kupambana na ugonjwa wa Malaria na mbu wanaoeneza ugonjwa huo.Akiongea katika kikao cha ngazi ya Makatibu Wakuu wa Wizara kilichohusu ushirikiano wa Kisekta katika Mapambano dhidi ya Malaria kilichofanyia Aprili 16,2024 jijini Dodoma katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Yonazi alisema lengo la kikao hicho ni kuhakikisha Serikali inatengeneza mfumo mzuri wa namna ya kupambana na malaria nchini ili kuweza kuokoa nguvu kazi ya Taifa la Tanzania na rasilimali zitakazotumika katika kutibu ugonjwa huo.
“Tunaamini kwamba tunapokuwa na Taifa ambalo halina Malaria tunaweza kuongeza tija katika uchumi na katika maendeleo kwa haraka katika nchi yetu, kwa hivyo nitoe wito kwa Makatibu Wakuu na wadau wote tunaoshirikiana kuhakikisha kwamba tunaongeza nguvu ili tuweze kupambana na ugonjwa wa Malaria na vilevile mbu waenezao ugonjwa huo,"alisisitiza Dkt. Yonazi.
Aidha, Katibu Mkuu Yonazi alitoa wito kwa Jamii ya Watanzania kuendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali ili kuhakikisha, jamii hizo zinapambana na mbu waenezao Malaria katika nyumba zao na mazingira yanayowazunguka.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Afya,Dkt. Ahmed Makuwani alisema, Serikali imepiga hatua kubwa sana katika kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kwa maambukizi ya asilimia (8.1%) kwa sasa tofauti na huko nyuma ambapo maambukizi yalikuwa zaidi ya marambili ya asilimia ya sasa,na kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kwa zaidi ya asilimia sabini (70%) kutoka mwaka 2015 tofauti na sasa ambapo vifo vitokanavyo na Ugonjwa wa Malaria ni 3,600 kwa mwaka.
“Lakini bado kuna maambukizi ya Malaria ambayo yanaleta madhara makubwa kwa hivyo sisi kama Serikali, tunahitaji kuongeza mikakati ambayo itaenda mpaka kwenye ngazi ya jamii lakini kila Wizara na kila sekta inatakiwa kushiriki kwa namna yake ili kuangalia namna gani bora ya kutimiza malengo ya kupunguza maambukizi zaidi ya Malaria na kuifanya Tanzania kuwa sehemu Salama,”alibainisha Dkt. Makuwani.

Kaimu Katibu Mkuu huyo pia aliitaja mikoa inayoonekana kuwa na maambukizi makubwa ya Malaria ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Tabora, Mtwara, Kigoma, Kagera na kusema kuwa Mikoa hii inakuwa na Afua mbalimbali ikiwa ni pamoja na Afua za kupambana na mbu kutoka kwenye mazalia yake na kuhakikisha kuwa kunakuwa na unyunyuziaji wa ukoko kwenye majumba ya watu, matumizi ya vyandarua na kuhakikisha wanaopatikana kuwa na Ugonjwa huo wanapata Tiba Stahiki ili wasitengeneze mzunguko mwingine wa maambukizi toka kwa mbu.

Awali akiongea kutoka Shirika la SWISS TPH linalofadhiliwa na ubalozi wa Uswisi nchini, Bi. Noela Kisoka alisema, shirika hilo limekuwa likitoa msaada wa kitaalam kwenye mambo mbalimbali yanayohusiana na Malaria, ikiwa ni pamoja na eneo la udhibiti wa mbu, masuala mazima ya ufuatiliaji na tathmini pamoja masuala ya upimaji na matibabu ya ugonjwa wa malaria (case management).
Aidha, alisema kuwa pamoja na afua hizo kuu katika mapambano dhidi ya Malaria shirika hilo pia limejikita katika kusaidia masuala ya kisekta, kwa kuwa ugonjwa huo nchini unatakiwa kutokomezwa kwa ushirikiano wa pamoja wa sekta tofauti akitolea mfano sekta ya madini, ujenzi, kilomo n.k na kuongeza kusema kuwa sekta hizo zote zina jukumu la moja kwa moja katika kutokomeza ugonjwa wa Malaria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news