Uzito uliozidi, hili janga la taifa

NA LWAGA MWAMBANDE

MIEZI kadhaa iliyopita Shirika la Afya Duniani (WHO) lilionya kuhusu kuongezeka kwa watu walio na uzito wa kupitiliza.
Picha na NYP.

Hali inayowaweka watu wengi katika hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukizwa.

WHO ambalo liliangazia unene duniani lilisema zaidi ya nusu ya watu duniani watakuwa na uzito wa juu au unene wa kupitiliza.

Ni kufikia mwaka 2035,ikiwa hatua madhubuti kudhibiti hali hiyo hazitachukuliwa.

Aidha,mataifa yanayoendelea na maskini barani Afrika na Asia yanatazamiwa kushuhudia hali hiyo.

Huku baadhi ya sababu zinazochangia hali hii zikitajwa ni ulaji na watu kushindwa kufanya mazoezi mara kwa mara.

Kutokana na changamoto hiyo, Serikali kupitia viongozi wake wakuu akiwemo Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kuwa, tatizo la uzito uliozidi na kiriba tumbo kwa sasa limekuwa janga la kitafa.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, janga hili la Kitaifa yafaa sasa tusimame imara kupambana nalo. Endelea;

1. Uzito uliozidi, na hivi viribatumbo,
Hatutaki ushahidi, jinsi vyatupiga kumbo,
Hiyo wala si akidi, kungurumisha mitambo,
Hili janga la taifa, bora tupambane nalo.

2. Ni uzito ulozidi, wa mwili wa si wa tumbo,
Wala hiyo siyo jadi, ya kuwa na hilo umbo,
Ni kwa ulaji zaidi, na zoezi kuwa fumbo,
Hili janga la taifa, bora tupambane nalo.

3. Mtu akula vizuri, chakula chenda kwa tumbo,
Na wala hana safari, mazoezi siyo jambo,
Mwili unazaa shari, hata afya kwenda kombo,
Hili janga la taifa, bora tupambane nalo.

4. Si vijana si wazee, wanacho kiribatumbo
Vile maisha ya chee, japo zinaimbwa nyimbo,
Kwamba vema watembee, kama vile ni mgambo,
Hili janga la taifa, bora tupambane nalo.

5. Kwa kulakula vibaya, chakula kujaza tumbo,
Mazoezi eti haya, kama wawania jimbo,
Matokeo ni mabaya, afya ni mbovu kitambo,
Hili janga la taifa, bora tupambane nalo.

6. Haya magonjwa magonjwa, yasoambukiza wimbo,
Mwili nguvu unavunjwa, kazi zawa ni mafumbo,
Jinsi watu wanagonjwa, hospitali kitambo,
Hili janga la taifa, bora tupambane nalo.

7. Kisukari saratani, yaongezeka kitambo,
Hatari sana mwilini, lazima tufanye jambo,
Kwa kwenda mazoezini, uzito uwe wa kambo,
Hili janga la taifa, bora tupambane nal

8. Vema kula kwa kiasi, chakula lishe cha tumbo,
Si kulipitiza kisasi, ulichokosa kitambo,
Uzito uwe kiasi, siyo wa kiribatumbo,
Hili janga la taifa, bora tupambane nalo.

9. Kwa afya kuwa vizuri, uzito wako ni jambo,
Vitu sukarisukari, hivyo pungua kitambo,
Wanga chumvi sikariri, mwilini vyaleta mambo,
Hili janga la taifa, bora tupambane nalo.

10. Wetu Waziri Mkuu, leo amesema jambo,
Tusikie la mkuu, tukinge viribatumbo,
Tusijevunjika guu, magonjwa yawe ni shombo,
Hili janga la taifa, bora tupambane nalo.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news