Watumishi Sekta ya Maji watakiwa kushirikiana

MWANZA-Watumishi Sekta ya Maji kote nchini wametakiwa kufanya kazi kwa kushirikiana bila kujali taasisi wanazotoka ili kuhakikisha dhamira ya Serikali ya kumtua Mama ndoo ya maji kichwani inafikiwa kikamilifu.
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Ndg. Wanyenda Kutta ametoa rai hiyo Aprili 15, 2024 katika kikao na Watumishi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mwanza.

"Hizi sio zama za kujitenga na kufanya kazi peke yenu; tunapaswa kuwa na utendaji wa pamoja kwani sote lengo letu ni moja la kuhakikisha wananchi katika maeneo tunayohudumia wanapata huduma ya majisafi na salama," amesisitiza Kutta.

Amesema kuwa ujio wake Mkoani Mwanza ni kuhakikisha anaendeleza dhana na chachu ya msisitizo wa Viongozi katika ngazi mbalimbali katika kuwataka watumishi wa Sekta ya Maji kutimiza wajibu wao kwa pamoja na kwa mmoja mmoja.
"Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunazitendea haki kazi zetu na Watanzania wenzetu na haşa kwa Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye ana imani kubwa na sisi Watumishi wa Sekta ya Maji katika wajibu wetu wa kumtua Mama ndoo kichwani na kuweza kuchangia uchumi wa nchi yetu. Haya pia yamekuwa yakisisitizwa na Waziri wetu Mhe. Jumaa Hamidu Aweso (Mb,)," amesema.

"Tusimuangushe Mhe. Rais na Waziri wetu, tuitendee Serikali yetu haki. Tusiwaangushe viongozi wetu na wananchi waliotupa dhamana ya kuwahudumia kwani wote wanatuamini tusivunje imani hiyo na hili linawezekana kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake ipasavyo," amesisitiza.

Amesema, Serikali kupitia Wizara ya Maji imepewa malengo kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya kuhakikisha ifikapo 2025 huduma ya maji kwa maeneo ya vijijini iwe imefikia asilimia 85 na maeneo ya mijini asilimia 95 na amesisitiza suala hilo litafikiwa kwa kufanya kazi kwa ushirikiano. Na kwamba inapasa hata vitendea kazi kama mitambo ya uchimbaji wa visima vitumike ipasavyo.

"Waziri wetu anafanya makubwa; inatupasa tuige mfano huo nasi sote kwa pamoja tuhakikishe hatuwi kikwazo kwa wananchi kupata huduma ya maji," amesema.Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Godfrey Sanga amemthibitishia Ndg. Kutta kuwa wepokea maelekezo na kuahidi kuhakikisha malengo yanafikiwa kikamilifu.

Amesema kwa Mkoa wa Mwanza Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji, zinafanya kazi kwa kushirikiana bila kujali kama lengo li kufikisha huduma mijini ama vijijini.

"Tunakuhakikishia Mkurugenzi maelekezo na salam kutoka kwa Waziri wetu, Mhe. Jumaa Aweso tumezipokea na tunaahidi kutokuwa kikwazo kwa wana Mwanza kupata huduma na hata sasa tunashirikiana na Bonde katika suala la uchimbaji wa visima," amesema Mhandisi Sanga.

Mkurugenzi Kutta yupo Mkoani Mwanza kwa ziara ya siku tatu ambayo imelenga kutembelea taasisi katika Sekta ya Maji; kuzungumza na watumishi na kuzipatia ufumbuzi changamoto za kiutumishi walizonazo watumishi ambao ni Rasilimali namba moja yenye thamani katika kuleta maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news