Waziri Dkt.Gwajima aikaribisha MEWATA kushirikiana na wizara

DAR ES SALAAM-Serikali imetoa wito kwa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania, MEWATA kufanya kazi kwa pamoja kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ili kutatua changamoto mbalimbali ndani ya Jamii zenye matokeo hasi kwenye afya.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, alipokuwa akifungua Mkutano wa 21 wa Mwaka wa chama hicho, Aprili 21, 2024 jijini Dar Es Salaam.

Waziri Dkt. Gwajima amebainisha kuwa, changamoto nyingi kwenye jamii hupelekea matokeo yenye athari za kiafya mathalani msongo wa mawazo, afya duni ya akili na hata ukatili wa kijinsia unaodhuru afya, ambapo msingi mkubwa ni jamii kutoelewa jinsi gani baadhi ya mitindo ya maisha, mila, tamaduni na desturi zao zina athari kubwa kwenye afya kuanzia umri wa awali wa mtoto, ujana hadi uzee.

"MEWATA kama taasisi ya madaktari wanawake ina nafasi ya kufanya mapinduzi makubwa kwenye jamii kwa kupeleka elimu na huduma. Mambo mengi tunayoyaona huku juu kama changamoto ikiwemo ukatili wa kijinsia, ndoa kuvunjika, watoto wa mitaani, mila kandamizi yanaweza kudhibitiwa iwapo MEWATA itaingia kwenye kutoa elimu ndani ya jamii na kutokomeza mizizi ya changamoto hizi,"amesema Dkt. Gwajima.

Aidha, ameiomba MEWATA kutumia taaluma zao kikamilifu bila aibu pale wanapohudumia wagonjwa, kuchambua hali ya ugonjwa na historia za maisha ya kijamii ili kubaini msingi wa tatizo la afya kutokana na maisha ya kijamii.
Kwa upande wake rais wa chama hicho, Dkt. Zaitun Bohari amesema kuna changamoto nyingi wanazopata wanawake ambazo hazizungumzwi kwenye jamii kutokana na mila na desturi kandamizi, hivyo kwa MEWATA ni changamoto mojawapo ya kufanyia kazi kuhakikisha inatoa elimu ya afya kwa wanawake hasa vijijini.

Baadhi ya wanachama wa MEWATA walioshiriki mkutano huo kutoka maeneo mbalimbali nchini, wameishukuru Serikali kwa ushirikiano na kuahidi kuendelea kutoa mchango kama chama cha kitaaluma kwa kuboresha afya ya mama na mtoto kwa ustawi wa jamii nzima.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news