Waziri Mkuu aipa heko DCEA kwa kazi nzuri udhibiti wa dawa za kulevya nchini

NA GODFREY NNKO

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ameipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa namna inavyodhibiti biashara ya dawa za kulevya nchini.
Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo Aprili 9, 2024 wakati wa hafla ya Futari aliyoiandaa kwa ajili ya watumishi wa ofisi yake na taasisi zake, Mlimwa jijini Dodoma.

"Upande wa Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya tunaye hapa, Bwana Lyimo (Aretas Lyimo) alishaanza kazi, amefanya kazi nzuri sana.

"Ameendesha operesheni,amekamata madawa, zaidi ya madawa tuliyowahi kuyakusanya miaka yote, ameenda shambani, mpaka kule Arusha akavuna cha Arusha chote (bangi) hongera sana.
"Lakini pia (Kamishna Jenerali Lyimo) amefanya maboresho kwenye sekta yake, tulipotoka tulikuwa tunaboresha, lakini Kamishna Jenerali ameboresha zaidi kwamba ofisi yake haiishi makao makuu ya nchi tu, ameshusha kwenye kanda na tayari wakurugenzi wameshaenda kwenye kanda.

"Zoezi la Kamishna Jenerali sasa litafanikiwa sana kwa sababu ameshusha watu ambao watasimamia operesheni zote, mipango yote ya kudhibiti na kukamata wazalishaji, wasafirishaji, watumiaji na wafanyabiashara,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo ikiwa,Kamishna Jenerali Lyimo tangu ateuliwe kuongoza nafasi hiyo Machi 16,2023 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na timu yake wamefanikiwa kudhibiti na kukamata shehena kubwa ya dawa za kulevya nchini.

Dawa hizo zinajumuisha zile za viwandani, mashambani na aina mpya ya dawa ambazo zinachipukia kwa sasa duniani.
Miongoni mwa operesheni zilizovunja rekodi
ni ile ya Desemba, mwaka jana ambapo DCEA ilikamata shehena kubwa ya dawa za kulevya aina ya Heroin na Methamphemine.

Katika tukio hilo, Kamishna Jenerali Lyimo aliwaeleza wanahabari jijini Dar es Salaam kuwa,kupitia operesheni walizozifanya kati ya Desemba 5 hadi 23, 2023 jumla ya kilo 3,182 za dawa hizo zikiwa kwenye vifungashio vya kahawa na majani ya chai zilikamatwa katika Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Iringa.

“Ukamataji huu umeokoa nguvu kazi yaani Tanzania tupo idadi ya watu milioni 60 hizi dawa zingefanikiwa kuingia sokoni basi zingeathiri si tu Watanzania bali hata mataifa mengine maana nyingine zilikuwa zikisafirishwa nchi nyingine,”alisema Kamishna Jenerali Lyimo.

Kamishna Jenerali Lyimo alisema, kiasi hicho cha dawa kilijumuisha kilo 2,180.29 za dawa aina ya Methamphemine na kilo 1,001.71 aina ya Heroin zilizokamatwa katika wilaya za Kigamboni, Ubungo na Kinondoni jijini Dar es Salaam na mkoani Iringa.
Pia, Watanzania hivi karibuni wameshuhudia operesheni kubwa ya kufyeka, kuteketeza mashamba ya bangi na mirungi katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa na Morogoro ambayo imekuwa ikiongozwa na Kamishna Jenerali Lyimo mwenyewe.

Hayo ni baadhi ya matukio wachache ambapo katika kipidi kifupi DCEA imekamata zaidi ya dawa hizo huku wahusika wakifikishwa katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.

Kuhusu DCEA

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015.

Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.

Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.

Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995, ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.

Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu tarehe 17 Februari, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.

Majukumu

Majukumu ya Mamlaka ni kufafanua, kuhamasisha, kuratibu na kutekeleza hatua zote zinazoelekezwa katika udhibiti wa dawa za kulevya.

Aidha,katika kutekeleza majukumu hayo,DCEA inafanya kazi zifuatazo;

i.Kusimamia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa, maazimio na makubaliano katika kudhibiti dawa za kulevya.

ii.Kuandaa na kutekeleza mpango wa Taifa wa kudhibiti dawa za kulevya.

iii.Kutengeneza miongozo inayoelezea tatizo la dawa za kulevya na madhara yake katika jamii;

iv.Kuboresha na kurekebisha sheria na kanuni za udhibiti wa dawa za kulevya;

v.Kuhamasisha udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya ikiwemo kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya, kusambaza taarifa kwa umma na juhudi nyingine za udhibiti;

vi.Kuchukua hatua stahiki za kupambana na biashara ya dawa za kulevya zikiwemo kukamata, kupekua na uchunguzi wa masuala yanayohusiana na dawa za kulevya.

vii.Kuzuia, kupeleleza na kuchunguza uchepushaji wa dawa za tiba zenye madhara ya kulevya pamoja na kemikali zilizosajiliwa kutoka kwenye vyanzo halali wakati huo huo kuhakikisha dawa hizo zinapatikana kwa matumizi ya tiba, biashara na mahitaji ya kisayansi;

viii.Kuanzisha mfumo thabiti wa ukusanyaji taarifa na uchambuzi katika ngazi ya taifa kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya;

ix.Kuhamasisha, kuratibu na kuhakikisha jitihada za ushirikiano wa kimataifa katika kudhibiti wa dawa za kulevya zinaimarishwa;

x.Kufanya, kuwezesha na kuratibu tafiti zinazohusiana na dawa za kulevya;

xi.Kuratibu na kuwezesha wadau wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya;

xii.Kuelimisha na kuhamasisha jamii kushiriki katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya;

xiii.Kutoa mafunzo kwa watendaji wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya, fedha haramu na kemikali bashirifu.

xiv.Kufanya uchunguzi wa sayansi jinai.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news