BoT:Mafunzo ya Elimu ya Fedha kuwakwamua wananchi kiuchumi

DAR-Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Yamungu Kayandabila, amesema mafunzo ya elimu ya fedha kwa wanaotoa elimu hiyo yatawasaidia wananchi kupata elimu sahihi na yenye ubora kuhusu matumizi ya fedha zao ili kujikwamua kiuchumi.
Dkt. Kayandabila ameyasema hayo alipokuwa akihutubia wahitimu 86 wa Mafunzo ya Cheti cha Ithibati ya Weledi wa Utoaji wa Elimu ya Fedha kwa Umma yaliyotolewa na Chuo cha Benki Kuu (BoT Academy) kuanzia tarehe 27 hadi 7, Juni 2024 katika ofisi za makao makuu ndogo, jijini Dar es Salaam.
“Tunaamini kuwa elimu na maarifa mliyopata kupitia mafunzo haya si kwa ajili ya maendeleo yenu binafsi tu, bali pia itakwenda kuwasaidia wananchi walio wengi, ambao hawana uelewa mzuri juu ya elimu ya fedha,” amesema Dkt. Kayandabila.

Aidha, ameongeza kuwa mafunzo hayo yatakuwa endelevu ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za teknolojia zinazokumba ulimwengu.
“Sekta ya fedha inapitia changamoto mbalimbali na kwa kiasi kikubwa changamoto hizo zinatokana na mabadiliko ya teknolojia. Kwa maana hiyo, wananchi wetu lazima wapate elimu hii endelevu ili wasiathirke na mabadiliko mbalimbali katika hiyo,” ameeleza.

“Tutahimiza watoa huduma za fedha waweke vikokotoo vitakavyowasaidia walaji kupiga hesabu za mikopo yao vizuri,” amesisitiza Dkt. Kayandabila.Naye, Meneja wa Huduma Jumuishi za Fedha Benki Kuu ya Tanzania, Bi. Nangi Massawe, amesema mafunzo hayo yatasaidia kutokomeza vitendo vinavyofanyika kinyume na taratibu katika sekta ya fedha.

“Tunatarajia kuwa na umma ulioelimika ili vitendo visivyo vya haki katika sekta ya fedha kama vile viwango vya juu vya riba, mikopo isiyolipika, udanganyifu, uhalifu wa mtandao, utakatishaji fedha na ukosefu wa uwajibikaji kwa watoa huduma za fedha vikose nafasi katika jamii,"amesema.

Akiongea kwa niaba ya wahitimu wa mafunzo hayo, Bw. Mark Peter, amesema, wao kama wahitimu wa kundi la kwanza wa mafunzo hayo, wameazimia kutoa elimu ya fedha kwa umma kwa weledi na umahiri sawasawa na sera, kanuni, mtaala na miongozo waliyopewa na serikali kupitia Benki Kuu.
Benki Kuu ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha elimu ya fedha inawafikia wananchi ikiwemo kutoa mafunzo yanayohusu elimu ya fedha ambapo kutokana na ukubwa wa nchi yetu, jukumu hili limekasimishwa kwa vyuo mbalimbali nchini, kikiwemo Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news