Masoud Pezeshkian ashinda urais Iran

NA DIRAMAKINI 

MGOMBEA urais mwenye msimamo wa wastani wa kisiasa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian ameshinda uchaguzi wa rais katika duru ya pili dhidi ya mhafidhina Saeed Jalili.
Hayo ni kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa Julai 6,2024 na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran.

Aidha, Msemaji wa Tume ya Uchaguzi nchini Iran,Mohsen Eslami amesema, Pezeshkian alipata zaidi ya kura milioni 16 na Jalili zaidi ya milioni 13 kati ya kura milioni 30 zilizopigwa.

Eslami aliongeza kuwa, idadi ya wapiga kura ilifikia asilimia 49.8 huku idadi ya kura zilizoharibika iliripotiwa kuwa zaidi ya 600,000.

Pezeshkian alisema kuwa, kura hiyo ilikuwa mwanzo wa ushirikiano na watu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Masoud Pezeshkian ambaye ni Mbunge mkongwe na waziri wa zamani wa Afya aliibuka kidedea katika duru ya pili ya uchaguzi ambao ulionekana mkali kwa kumshinda msuluhishi wa zamani wa mazungumzo ya nyuklia, Saeed Jalili.

Baada ya wizara kutangaza matokeo ikiashiria kukamilika kwa uchaguzi ambao ulishuhudia ushiriki mkubwa wa wapiga kura licha ya changamoto nyingi.

Katika matamshi yake ya kwanza tangu kutangazwa mshindi, Pezeshkian alitoa salamu zake kwa Wairan wote.

"Tunanyoosha mkono wa urafiki kwa kila mtu, sisi sote ni watu wa nchi hii, tunapaswa kutumia kila mtu kwa maendeleo ya nchi," alisema kupitia televisheni ya Taifa.

Baadaye, aliandika katika mtandao wake wa X (zamani Twitter) kuwashukuru watu wa Iran kwa imani yao, na kuahidi kutowaangusha.

"Wapendwa watu wa Iran, uchaguzi umekwisha na huu ni mwanzo tu wa umoja wetu. Njia ngumu mbeleni haitakuwa laini isipokuwa kwa urafiki wenu, huruma na uaminifu.

"Ninawanyooshea mkono na ninaapa kwa heshima yangu kwamba sitawaacha peke yenu kwenye njia hii."

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani Ahmad Vahidi pia alitoa shukrani zake kwa wapiga kura na kumpongeza Pezeshkian kwa ushindi wake.

"Ninamshukuru Mwenyezi Mungu, uchaguzi wa 14 wa rais ulimalizika kwa usalama na utulivu, ushindani mkubwa wa wagombea na ushiriki wa zaidi ya watu milioni 30 wa Iran ulionekana, na rais wa tisa wa Iran alichaguliwa. Bw. Masoud Pezeshkian amechaguliwa kuwa mkuu wa Serikali ya 14, na ninampongeza," Vahidi alisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news