DAR-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameondoka nchini leo Alhamisi, Septemba 19, 2024 kwenda Marekani ambako atamwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79).
Mkutano huo unaotarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 20-26, 2024, utafanyika jijini New York, Marekani ambapo masuala ya kiuchumi, biashara, nishati, siasa, mazingira, afya, vijana na watoto yatajadiliwa. Masuala mengine ni ya maji, bahari, athari za hali ya hewa na haki za binadamu.
Katika mkutano huo ambao hufanyika kila mwaka, viongozi wa nchi mbalimbali wanatarajiwa kushiriki mijadala tofauti chini ya mada kuu ambayo ni “Hakuna kuachwa nyuma yeyote: Kushirikiana pamoja kuendeleza amani, maendeleo endelevu na heshima ya binadamu kwa vizazi vya sasa na vijavyo" (Leaving no one behind: Acting together for the advancement of peace, sustainable development and human dignity for present and future generations).
Mbali na kukuza diplomasia, ushiriki wa Tanzania kwenye mkutano huo unatoa fursa ya nchi kuwasilisha maslahi yake katika jukwaa la kimataifa, kujifunza kutokana na uzoefu wa nchi nyingine na pia kuwasilisha ajenda na mipango ya maendeleo ya nchi kwa jamii ya kimataifa.