NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa, hadi kufikia Ijumaa ya wiki iliyopita imetoa leseni kwa taasisi zaidi ya 2,450 za Daraja la Pili kati ya taasisi 3,075 zilizotuma maombi.
Afisa Mkuu Mwandamizi, Idara ya Usimamizi wa Huduma ndogo za Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Deogratias Mnyamani ameyasema hayo leo Februari 26,2025 mkoani Mtwara.
Ni katika siku ya pili ya semina kwa waandishi wa habari za uchumi kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam,Ruvuma na Zanzibar wakati akielezea mafanikio na changamoto za usimamizi wa sekta ya huduma ndogo za fedha.
"Benki Kuu inaendelea kutoa leseni na kusimamia taasisi za Daraja la Pili ambazo hadi kufikia sasa zaidi ya taasisi 2,450 zimeshapatiwa leseni na maombi yaliyopokelewa yanafikia 3,075."
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 imepewa jukumu la kutoa leseni,kudhibiti na kusimamia taasisi za huduma ndogo za fedha nchini.
Kifungu cha 16 cha sheria hiyo kinasema mtu yeyote nchini hawezi kutoa huduma ndogo za fedha bila kuwa na leseni ya Benki Kuu ya Tanzania.
Sheria hiyo imegawanya watoa huduma ndogo za fedha katika makundi manne.
Kwa mujibu wa Bw.Mnyamani makundi hayo ni taasisi za kibenki zinazotoa huduma za fedha (microfinance banks).
Pia, amesema kundi la pili ni watoa huduma ndogo za fedha wasiopokea amana.
Bw.Mnyamani amesema, kundi la tatu linasimamiwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini kwa kukasimishwa mamlaka na Benki Kuu.
Kwa upande wa kundi la nne ambalo ni Vikundi vya Kijamii vya Huduma Ndogo za Fedha (VICOBA) ambavyo vinafikia 60,346 hadi kufikia Ijumaa iliyopita.
Mnyamani amesema, kundi la nne linasimamiwa na mamlaka za Serikali za mitaa nchini.
Amesema katika kipindi cha miaka sita ya utekelezaji wa sheria hiyo kuna mapokeo chanya pamoja na kanuni zake.
Mnyamani amesema, mafanikio mengine ni kuimarika kwa mahusiano kati ya watoa huduma na Benki Kuu.
"Pia, kuna mwamko mkubwa wa watoa huduma ndogo za fedha kutuma maombi ya leseni na tumefanya ukaguzi kwa watoa huduma zaidi ya 300 mpaka sasa."


