Naibu Waziri Chumi ashiriki Mkutano wa Nane wa Bahari ya Hindi nchini Oman

MUSCAT-Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bal. Mohamoud Thabit Kombo ameshiriki Mkutano wa Nane wa Bahari ya Hindi ulioanza jijini Muscat, Oman tarehe 16 Februari 2025.
Mkutano huo wa siku mbili ulifunguliwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Oman na India Pamoja na Rais wa Taasisi ya India Foundation.

Akizungumza katika Mkutano huo, Mhe. Chumi ameeleza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kulinda rasilimali za Bahari.

Mheshimiwa Chumi pia amehimiza matumizi sahihi na endelevu ya bahari na kusisitiza umuhimu wa nchi za bahari ya Hindi kuendelea kushirikiana ili kutatua changamoto zinazozikumba nchi hizo ikiwemo uvuvi haramu, uharamia na uharibifu wa mazingira na ekolojia ya bahari.
Katika tukio lingine, pembezoni mwa Mkutano huo, Mhe. Chumi amekutana na kuzungumza na viongozi mbalimbali walioshiriki mkutano huo ambapo amekutana na Waziri wa Madini, Uchumi wa Buluu na Masuala ya Bahari wa Kenya, Mhe Hassan Ali Joho.

Wakati wa Mazungumzo na Waziri Joho, viongozi hawa walijadiliana namna ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa kindugu na kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Kenya. Viongozi hao wamekubaliana kukamilisha Hati za Makubaliano zilizopo ili masuala ya usafirishaji wa baharini na uchumi wa buluu yachangie maendeleo ya watu na nchi hizo.
Aidha, Mhe. Chumi alikumbusha Kenya kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya Mkataba wa Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na kuleta maafisa wao wa KRA kufanya kazi huku Tanzania kama tulivyokubaliana.
Vilevile, aliwakumbusha kutoa kibali cha kuruhusu ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania kuruhusiwa kupeleka mizigo katika miji mingine ya Kenya bila kuhitaji kutafuta kibali maalum inapotokea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news