PWANI-Jeshi la Polisi limesema video inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikionesha kijana akikamatwa kwa nguvu ni tukio la ukamataji lililofanywa na Askari Polisi Februari 20,2025 katika eneo la Maili Moja Mkoa wa Pwani.
Taarifa iliyotolewa Februari 22,2025 na Msemaji wa Polisi imesema, mtuhumia huyo Rajabu Hassan alikuwa anatafutwa kutokana na tuhuma mbalimbali za kujihusisha na matukio ya uporaji kwa kutumia pikipiki ikiwa imekunjwa namba za usajili (plate number) na wakati mwingine ikiwa haina namba ya usajili kwa jina maarufu Vishandu.“Hata wakati anawakimbia Polisi walipojaribu kumkamata na kuwakimbia katika eneo la Mwendapole pikipiki aliyokuwa anandesha ilikuwa haina namba ya usajili, baadaye Polisi walipofanikiwa kumkamata katika eneo la Maili Moja ilikuwa haina namba ya usajili.
“Wakati wa ukamataji alianzisha vurugu ili kukaidi ukamataji pamoja na Askari Polisi kujitambulisha kwake, hata hivyo walifanikiwa kumkamata na kumfikisha Kituo cha Polisi Kibaha ili kuendelea na taratibu nyingine za kisheria kuhusiana na tuhuma zinazomkabili, ndugu zake nao wanazo taarifa kuwa anashikiliwa katika kituo hicho.”