CHADEMA ndiyo kama ulivyosikia,wagombea watoa waraka mzito

KATIKA kile kinachoweza kufasiriwa kama dalili za kuporomoka kwa umoja na mshikamano ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), waraka mzito wa ushauri umetolewa na wagombea wa ubunge wa mwaka 2020 na watia nia wa mwaka 2025, wakimlenga moja kwa moja Katibu Mkuu wa CHADEMA huku wakionyesha tofauti kubwa ya kifikra na kimkakati na viongozi wakuu wa chama hicho.
Waraka huo, uliosainiwa na wawakilishi 55 wa watia nia zaidi ya 200, unaweka bayana mgawanyiko mkubwa uliopo ndani ya CHADEMA kati ya viongozi wakuu wa chama hicho na wafuasi wake wa ngazi za kati na chini.

Kauli za Lissu na Lema zazua hofu

Wagombea hao wamemkosoa vikali Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Tundu Lissu, kwa kutoa kauli za kuwabagua wanachama wenye mtazamo tofauti kuhusu kampeni ya "No Reforms, No Elections".

Kwa mujibu wa waraka huo, kauli ya Lissu kwamba wale wasioamini katika "No Reforms, No Elections" ni wana-CCM na vibaraka wao, imetafsiriwa kama tishio kwa uhuru wa maoni ndani ya chama.

Aidha, kauli ya Godbless Lema, mjumbe wa Kamati Kuu na mwenyekiti wa kamati ya uchangishaji wa kampeni hiyo, aliyesema wazi kuwa “wote wanaotaka ubunge au udiwani bila reforms waondoke CHADEMA”, imezua hofu ya kufukuzwa kwa wanachama wenye mawazo tofauti, jambo linalodhihirisha ukosefu wa demokrasia ya kweli ndani ya chama hicho kinachodai kuwa mtetezi wa demokrasia.

Maria Sarungi ametajwa kama kiini cha mvurugano

Waraka huo pia unamtaja mwanaharakati Maria Sarungi kama mmoja wa watu wanaoingilia masuala ya ndani ya CHADEMA, licha ya kutokuwa mwanachama.

Kauli zake kwenye mitandao ya kijamii zimetafsiriwa kama tishio jingine kwa uhuru wa maoni wa wanachama, huku chama kikishindwa kuchukua hatua yoyote dhidi yake, hali inayoibua maswali kuhusu uhusiano wake wa karibu na baadhi ya viongozi wa juu wa CHADEMA.

Kukataa mpango wa kususia uchaguzi

Wagombea hao wamesema wazi kuwa hawaungi mkono mpango wa CHADEMA wa kususia uchaguzi wa mwaka 2025 endapo mabadiliko ya katiba na sheria za uchaguzi hayatapatikana.

Wameutaja mpango huo kama wa kiholela, usio na msingi wa kikatiba, na wenye madhara makubwa kwa mustakabali wa chama. Kwa mujibu wao, kutoshiriki uchaguzi kutakuwa sawa na kujitoa rasmi kwenye ulingo wa kisiasa na kutoa nafasi kwa CCM kuendelea kutawala bila upinzani wa maana.

Madhara ya kutoshiriki uchaguzi

Katika maelezo yao, wagombea hao wameorodhesha madhara lukuki yanayoweza kuikumba CHADEMA endapo haitashiriki uchaguzi, yakiwemo:

- Kupoteza wanachama na viongozi wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali,

- Kupungua kwa mvuto kwa umma,

- Kupoteza ruzuku kutoka serikalini,

- Kuathiri ari ya kuchangia chama,

- Na hatimaye kupoteza kabisa nafasi yake katika siasa za Tanzania.

Hitimisho: CHADEMA imegawanyika

Waraka huu unathibitisha kile ambacho wachambuzi wa siasa wamekuwa wakikisema kwa muda mrefu: CHADEMA si tena chama chenye umoja wa ndani.


Viongozi wake wakuu wamekuwa wakitoa matamko ya vitisho, kudharau wanachama wa kawaida na kutishia kuwafukuza wale wenye maoni tofauti.

Demokrasia ndani ya chama hicho imesambaratika, na sasa kumeanza kuonekana waziwazi kuwa CHADEMA ni chama kinachoongozwa kwa matamko ya watu wachache, huku wafuasi wake wakizidi kukata tamaa na kupoteza imani.

Kwa hali hii, ni wazi kuwa CHADEMA iko katika mwelekeo wa kujimaliza yenyewe kabla hata ya CCM kuingilia kati. Wakati ambapo vyama vingine vya upinzani vinajipanga kushiriki uchaguzi na kupambana na mfumo dhalimu, CHADEMA imezama kwenye migogoro ya ndani, ajenda zisizoeleweka, na mapambano ya madaraka yaliyojificha kwenye kivuli cha "reforms".

Je, CHADEMA itaweza kujinasua katika mgogoro huu mkubwa wa kiuongozi na kiitikadi? Au hii ndiyo mwanzo wa mwisho wa chama kilichowahi kuwa matumaini ya wengi? Muda utaamua.





Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news