DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba ameshiriki katika kikao cha hitimisho la majadiliano kati ya Serikali ya Tanzania na timu ya wataalam kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Kikao hicho kilifanyika tarehe 17 Aprili 2025 katika ofisi za BoT, jijini Dar es Salaam, na kuongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.
Majadiliano hayo yamefanyika kufuatia kukamilika kwa tathmini ya awamu ya tano ya utekelezaji wa Mpango wa ‘Extended Credit Facility’ (ECF) ambao unahusisha mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii.
Vilevile, tathmini hiyo ilijumuisha awamu ya pili ya utekelezaji wa Mpango wa Resilience and Sustainability Facility (RSF), unaolenga kuisaidia Tanzania kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Nchemba alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa programu hizo kwa umakini mkubwa.
Alieleza kuwa jumla ya thamani ya programu hizo mbili ni Dola za Kimarekani bilioni 1.832, ambapo kiasi cha Dola bilioni 1.1 kimetengwa kwa ajili ya kuimarisha uchumi kupitia sekta za uzalishaji, na Dola milioni 786 kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Programu hizo zinatarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka wa fedha 2022/2023 hadi 2025/2026.

Naye, Bw. Nicolas Blancher, alithibitisha kuwa tathmini ya awamu ya tano imeonesha mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mpango wa ECF na RSF.