Makamu wa Rais atoa rai kwa wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu

DODOMA-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa wazazi hususani wakinamama kuwaongoza watoto wao hasa vijana kuacha tabia ya kushabikia vurugu wakati wa kampeni na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu.
Makamu wa Rais ametoa rai hiyo mara baada ya kushiriki Ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege Dodoma.

Amewasihi Watanzania kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa amani na utulivu kwa kuwa vurugu sio sehemu ya jadi ya Watanzania.
Aidha,Makamu wa Rais ametoa wito kwa wote watakaopata dhamana ya kusimamia uchaguzi kuhakikisha wanazingatia sheria na miongozo watakayopewa pamoja na kutenda haki kwa wote watakaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.

Halikadhalika, Makamu wa Rais amewasihi watumiaji wa vyombo vya moto kuwa na busara na umakini katika matumizi ya vyombo hivyo ili kuepusha kupoteza Maisha ya watu barabarani.

Makamu wa Rais amewatakia heri na baraka watanzania wote katika kusherehekea Sikukuu ya Pasaka na kuwasihi kusherehekea kwa amani na furaha.
Ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na Mwenza wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango imeongozwa na Padre Dionis Paskal Safari.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news