Mkutano wa 17 wa IAWJ wahitimishwa Afrika Kusini

NA MARY GWERA
Mahakama-Cape Town

MKUTANO wa 17 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) umehitimishwa huku wanachama wa Chama hicho wakisisitizwa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu.
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Mhe. Barke Sehel (katikati) akimpatia zawadi ya kitenge cha Chama hicho Jaji Mkuu wa Afrika Kusini, Mhe. Mandisa Muriel Maya (kushoto). Anayeshuhudia kulia ni Makamu Mwenyekiti wa TAWJA ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mhe. Victoria Nongwa.
Jaji Mkuu wa Afrika Kusini, Mhe. Mandisa Muriel Maya (wa tatu kushoto) akifurahia zawadi aliyopatiwa na Mwenyekiti wa TAWJA, Mhe. Barke Sehel (wa pili kulia).
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Mhe. Barke Sehel (kushoto) akimpatia zawadi Rais wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) aliyemaliza muda wake, Mhe. Binta Nyako.

Akifunga mkutano huo mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwakilishi wa Jaji Mkuu wa Afrika Kusini ambaye ni Jaji wa Mahakama Kikatiba ya Nchi hiyo, Mhe. Nonkosi Mhlantla aliwataka washiriki wa mkutano huo kujithamini na kujipenda sambamba na kutosahau waliyojifunza wakati wote wa mkutano huo.

“Nawasihi kutosahau kupitia mliyojifunza mtapata uzoefu mzuri, Majaji mbalimbali walipata nafasi ya kuchangia uzoefu wao juu ya namna wanavyoshughulikia mashauri yanayohusu vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na mauaji ya wanawake, hivyo ni muhimu kujifunza na kuyaishi yote mazuri tuliyoyapata,” alisema Mhe. Mhlantla.
Mwakilishi wa Jaji Mkuu wa Afrika Kusini ambaye ni Jaji wa Mahakama Kikatiba ya Afrika Kusini, Mhe. Nonkosi Mhlantla akifunga Mkutano wa 17 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Cape Town nchini Afrika Kusini.
Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) wakiwa katika picha ya pamoja siku ya mwisho ya Mkutano wa 17 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Cape Town nchini Afrika Kusini (CTICC).
Rais mpya wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ), Mhe. Maria Filomena D. Singh akizungumza jambo wakati wa mchapalo wa Chama hicho uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Cape Town (CTICC).
Jaji huyo aliwakumbusha Majaji na Mahakimu wanawake kujipenda na kujithamini kwanza ambapo alisema, “ni muhimu kujipenda na kujithamini, kufanya hivyo sio ubinafsi bali ni muhimu kufanya hivyo ili tuwe katika nafasi nzuri ya kutekeleza vizuri majukumu yetu ipasavyo,” alisisitiza.

Aidha, Jaji Mhlantla alisema kuwa, bado Mahakama nyingi hazina mbinu za kiusalama katika kuwalinda wahanga wa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia huku na kusema kwamba kuna haja ya kuchukua hatua thabiti ili kuwalinda watu hao.

Mgeni Rasmi huyo alizikumbusha pia nchi wanachama wa IAWJ kufanya uanaharakati ndani ya Mahakama hususani unaohusiana na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hususani akili unde ili kushughulikia matatizo mbalimbali yaliyopo ndani ya Mahakama ambayo ni pamoja na mlundikano wa mashauri.

Wakati wa mkutano huo uliofanyika kwa siku nne mada mbalimbali ziliwasilishwa ambazo ni pamoja na Majaji wanawake wanaongoza kuleta mabadiliko katika Mahakama za Kimataifa, Wanawake katika Uongozi-Mahali pa Kazi Usalama kwa Maafisa wa Mahakama, Ubaguzi na biashara haramu ya binadamu na nyingine.

Mada nyingine iliwasilishwa na Mhe. Edith Mwalukasa, Hakimu kutoka Mahakama ya Mwanzo Bagamoyo Tanzania mada hiyo ilijikita kuzungumzia ‘Athari za teknolojia katika masuala ya ukatili wa kijinsia.’
Picha mbalimbali za matukio yaliyojiri wakati wa Mkutano wa 17 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Cape Town nchini Afrika Kusini kuanzia tarehe 09 hadi 12 Aprili, 2025.(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Cape Town).

Aidha, wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa Chama hicho, wanachama wa IAWJ walifanya uchaguzi na kumchagua Rais mpya wa Chama hicho ambaye ni Mhe. Maria Filomena D. Singh kutoka nchini Morocco.

Mkutano huo ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili umeazimia kuwa, Mkutano ujao wa mwaka 2027 utafanyikia nchini Canada.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news