DAR-Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba (Fireman) amesema, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu hana ubavu wa kuzuia Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba,mwaka huu.
Amesema, lengo la kuendesha kampeni ambayo tayari imeshafia njiani ni ili kuficha aibu kwa sababu yeye na chama chake hawana fedha za kuingia katika uchaguzi.
"Kuhusiana na madai ya Tundu Lissu aliyojibu G55 kwamba mfumo atakaoutumia wao kutoingia kwenye uchaguzi na hili kuzuia uchaguzi ni kuandamana siku ya uchaguzi ni jambo ambalo haliwezekani."
Temba ameshangaa Lissu ambaye ni wakili mbobezi kuyatumia maneno hayo akiamini kuna kitu au jambo ambalo analificha nyuma ya pazia.
"Lissu anashindwa tu kuonesha hana fedha na watu wengi walimpinga wakati akigombea wakasema Lissu ni maskini, hawezi kukiongoza chama kikubwa.
"Sasa inaonekana wazi kwamba kinachomtesa Lissu ni umasikini, ameshika kazi ambayo inatakiwa ishikwe na matajiri.
"Maono yamepotea,chama hakina fedha, anaogopa kuishia kwenye aibu, kuaibika na kuangukia pua, kushindwa vibaya na Samia Suluhu Hassan wakilinganisha na kipindi kile cha nyuma alichogombea.
"Lissu ameamua kusimamia kwenye njia ambayo haina kichwa wala miguu, hata mtoto wa darasa la saba fomula hiyo atakukatalia."
Temba amesema,mwaka wa Awamu ya Pili ya uchaguzi uliomrudisha Muhammadu Buhari nchini Nigeria, "wakati wa uchaguzi nilibahatika kuwa katika mji mmoja unaitwa Benin huko Nigeria.
"Nilivyokuwa Benin siku ya uchaguzi katika hoteli niliyokuwa nimekaa, tulitangaziwa kwamba tusitoke nje kwa sababu Waibo, watu wa Biafra ambao wanahitaji kujitenga kwa muda mrefu walikuwa wameupinga ule uchaguzi na kiongozi wao, kwa kuwa kule kuna viongozi vyama vyao havina shida, ukabila chama kinaweza kuwa na ukabila, lakini chama cha siasa.
"Chama hicho ambacho kina Waibo wengi ambao walikuwa wamepinga na kususia na kusema wangeuzuia uchaguzi ule, walijitahidi sana kuzuia uchaguzi na watu wengine walikuwa wakitoka na silaa, baadhi ya wapinzani na wanapiga risasi juu baadhi ya mitaa, lakini hawakufaulu, uchaguzi ulifanyika."
Amesema, licha ya baadhi ya mitaa kuwa na watu wachache, mwisho wa siku kura zilipigwa zikakusanywa kwa ajili ya kumchagua Rais.
Temba amesema, kitendo cha Waibo kukataa kwenda kwenye uchaguzi kilisababisha Muhammadu Buhari akashinda kwa kishindo.
"Hicho ndicho ambacho Lissu anataka kukifanya sasa, atazuia watu wangapi wakati sheria yetu ya uchaguzi itafanyika ili kumtangaza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Ile hata akipata kura moja nchi nzima anatangazwa kuwa Rais, hata Dar es Salaam tu wakapiga kura watu laki tano, akapata kura laki tano au laki nne zinamfaa na zinamtosha kuwa Rais, kutokana na sheria ilivyo, sasa bado Tume ya Uchaguzi itaangalia zile kura alizopata Samia.
"Dar es Salaam kapata kura laki mbili, Mwanza kapata laki mbili, Dodoma akapata laki moja, Mbeya akapata laki mbili, Moshi akapata elfu 50, Arusha akapata laki moja, wakijumuisha nchi nzima zikapatikana labda milioni 3, anakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Sasa, Lissu aje hadharani aseme, awaambie CHADEMA na asiwadanganye kwamba kama atazuia, lakini wengine wakaweza kupiga kura kwenye makambi ya jeshi, makambi ya polisi, sehemu nyeti za viongozi na sehemu nyingine ambazo hawezi kufika kwa ajili ya kuzuia kwa sababu hao watu wanaonesha wapo ambao wanataka kuzuia.
"Lissu analazimisha atazuia wakati tangu amekuwa kiongozi hana watu waliomuhakikishia kuwa, ana uwezo wa kumzuia ambao ana majina au wanaonekana hata kwa jamii kwamba wanazuia zaidi ya vijana wasio na ajira walioko mijini huku vijijini atawazuia vipi.
"Aje aseme vijijini watazuia vipi ambapo huko vijijini hakuna vijana wenye uelewa, hawana simu za smartphone wala hawana TV, wamemsikia wapi kwamba amezuia wakati watu hao wanajua kila baada ya miaka mitano kuna uchaguzi na wamejiandikisha.
"Mbona hawakuzuia wakati wanajiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura? Lissu angekuwa kweli anataka kuzuia uchaguzi angezuia watu wasijiandikishe."
Amesema, kama angehamasisha watu wasijiandikishe hapo angefaulu kwani pasipokujiandikisha, watu hawawezi kupiga kura.
"Sasa watu wamejiandikisha, wanazuia vipi, Je? Tume ya Uchaguzi ikija na mbinu ya kuonesha kwamba watu wanaweza kupiga kura majumbani mwao kwa kutumia App na watu wakawa wanapiga kura wakiwa nyumbani kama huko Ulaya atafanyaje?.
"Na watu wanajulikana wapo kwenye Daftari, wanapiga kura mara moja na mfumo ukaonesha, endapo Tume ya Uchaguzi itakuja na mfumo huo wa mtu kupiga kura na wafungwa wakapiga kura kule ndani atawazuia vipi? Wasipige kura ili wamchague Samia.
"Kwa hiyo, bado Tundu Lissu hoja na maswali yake hayana mashiko na hayajajaa kwa sababu kuna wafungwa wanaweza wakapiga kura kama sheria itakuwa imeelekeza hivyo, atawazuiaje kwa hiyo bado Tundu Lissu hana uwezo wa kifedha na amekwama ndicho kinachomfanya aseme kwamba azuie uchaguzi.:
