VATICAN-Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani,Papa Francis amefariki dunia akiwa mjini Vatican leo Jumatatu ya Aprili 21,2025 akiwa na umri wa miaka 88.

Mwadhama Kardinali Farrell ametangaza kwa masikitiko kifo cha Baba Mtakatifu Francis akieleza;
"Ndugu wapendwa, kwa huzuni kubwa sina budi kutangaza kifo cha Baba Mtakatifu Francisko''.
"Saa 7:35 asubuhi ya leo (majira ya Roma), Askofu wa Roma, Francis, alirudi nyumbani kwa Baba. Maisha yake yote yaliwekwa wakfu kwa huduma ya Bwana na Kanisa Lake."
"Alitufundisha kuishi maadili ya Injili kwa uaminifu, ujasiri na upendo wa ulimwengu wote, hasa kwa ajili ya maskini zaidi na waliotengwa zaidi.
"Kwa shukrani nyingi sana kwa ajili ya kielelezo chake kama mfuasi wa kweli wa Bwana Yesu, tunaipongeza roho ya Papa Francisko kwa upendo wa huruma usio na kikomo wa Mungu Mmoja na wa Utatu."
Aidha,kifo cha Papa kimekuja chini ya saa 24 baada ya kujitokeza kwenye Uwanja wa St Peter's Square mjini Vatican kwa ajili ya Jumapili ya Pasaka.
Kiongozi huyo alihudumu kama papa kwa miaka 12, baada ya kuchaguliwa kwake Machi 13, 2013 kufuatia kujiuzulu kwa mshtuko kwa mtangulizi wake Benedict XVI.
Papa, ambaye sehemu ya pafu moja ilitolewa akiwa na umri wa miaka 20 alikuwa amepambana na matatizo ya afya kwa miaka mingi.
Februari 14, 2025, Papa Francis alilazwa katika hospitali ya Agostino Gemelli, Roma ambapo alifanya vipimo vya kitaalam na kuanza matibabu ya dawa baada ya vipimo vya kwanza kuonesha kuwa ana maambukizi kwenye njia ya upumuaji.
Historia ya Papa Francis
Papa Francis anatambulika kwa jina la ubatizo kama Jorge Mario Bergoglio na alizaliwa Desemba 17, 1936 mjii Buenos Aires, Argentina.
Aidha, alikuwa ni mtoto wa wahamiaji kutoka Italia ambapo kabla ya kujiunga na seminari, alifanya kazi kama mkemia.
Papa Francis alijiunga na Shirika la Wajezuiti mnamo mwaka 1958 na kupewa daraja la upadri mnamo mwaka 1969.
Alihudumu katika nyadhifa mbalimbali ndani ya Kanisa nchini Argentina ikiwa ni pamoja na kuwa Askofu Mkuu wa Buenos Aires.
Papa Francis aliteuliwa kuwa Kardinali mnamo mwaka 2001 na Papa Yohane Paulo II na alichaguliwa kuwa Papa mnamo Machi 13, 2013, kufuatia kujiuzulu kwa Papa Benedikto XVI.
Aidha,alichagua jina la Francis kwa heshima ya Mtakatifu Francis wa Asizi.Vilevile Papa Francis ni mmoja wa Mapapa wachache waliozaliwa nje ya Ulaya. Hasa, yeye ndiye wa kwanza kutoka Amerika.
Kabla yake, alikuwapo Papa Gregori wa Tatu, ambaye alitoka Syria, katika karne ya 8, ndiye alikuwa Papa wa mwisho kutoka nje ya Ulaya.