Serikali itaondoa vikwazo vyote vinavyochangia kukwamisha uendeshaji wa biashara hapa nchini-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameahidi Serikali kuondoa vikwazo vyote vinavyochangia kukwamisha uendeshaji wa biashara hapa nchini.
Rais Dkt. Mwinyi amesema hayo alipoizindua
Sera ya Biashara ya mwaka 2024 na Mpango wa Utekelezaji, Ripoti ya Tathmini ya Mazingira ya Ufanyaji Biashara ya mwaka 2024.

Hafla imefanyika leo Aprili 30,2025 New Amani Hotel Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi,Zanzibar.

Amesema,Wizara ya Biashara imefikia hatua hii kwa ajili ya kuweka mazingira rafiki na rahisi ya ufanyaji wa biashara na ukuzaji wa sekta ya biashara nchini.
"Uzinduzi huu utatuwezesha pia kuimarisha uzalishaji wa bidhaa kwa viwanda vya ndani vilivyopo na kuanzisha viwanda vipya, na hivyo kutuwezesha kuweza kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana."

Pia,amesema itaongeza mapato ya Serikali pamoja na kupunguza utegemezi wa uagizaji bidhaa kutoka nchi za nje.

"Napenda kutumia fursa hii kuipongeza Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kusimamia maendeleo ya sekta ya Biashara na Viwanda ili kuhakikisha kuwa biashara inafanyika kwa urahisi na bila ya urasimu pamoja na kuhakikisha kuwa mazingira mazuri ya uwekezaji katika Biashara na viwanda yanazingatiwa.

"Aidha, nawapongeza wale wote walioshiriki kuandaa vitabu hivi tunavyovizindua leo.

"Vitabu hivi vinategemewa sana katika kukuza sekta ya biashara kwani vitawasaidia wafanyabiashara kupata uwelewa kuhusiana na mazingira ya ufanyaji wa biashara na kuzisaidia taasisi kujitathmini kuhusu utekelezaji wa majukumu yao ya kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara hapa nchini."
Vilevile, Rais Dkt.Mwinyi ameishukuru Taasisi ya Trademark Afrika kwa ushirikiano wao na juhudi wanazozichukua za kuisaidia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.

Ni katika kufanikisha ukuaji wa sekta ya biashara ikiwemo ya kuiwezesha Wizara kufanya mapitio ya Sera ya Biashara ya mwaka 2006 na kuandaa Sera mpya ya Biashara ya mwaka 2024.

Sambamba na kusaidia kuandaa Taarifa ya mazingira bora ya ufanyaji biashara ya mwaka 2024 kwa kuwashirikisha wataalamu wa ndani.

Amesema,uandaaji wa Sera Mpya ya Biashara na Tathmini ya Mazingira ya Ufanyaji biashara ni hatua ya kufanikisha ahadi ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 ibara ya 157 inayoitaka Serikali kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji wa biashara.

"Hivyo Sera ya biashara ya mwaka 2024 ni matokeo ya mapitio ya Sera ya Biashara ya mwaka 2006.

"Sera hii mpya imelenga kuhakikisha kuwa Wafanyabiashara wanakuwa na uwanja mpana wa kufanya biashara zao kiushindani na kuweza kushiriki vizuri katika kufanya biashara kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi sambamba na kuongeza ushindani wa mauzo nje ya nchi ili kuongeza wigo wa bidhaa kufikia masoko mapya."
Rais Dkt.Mwinyi amesema,Ripoti ya Tathmini ya Mazingira ya Ufanyaji Biashara (Zanzibar Blue Print) iliyoandaliwa mwaka 2024 ina lengo la kuimarisha biashara na kuondosha urasimu.

"Tathimini hii imeweka mapendekezo ya kutatua changamoto katika makundi matatu makuu ambayo ni Sera zinazohusiana na biashara, sharia na na Taasisi zinazosimamia Biashara."

Kwa upande wa taasisi zinazosimamia biashara, ripoti imetoa mapendekezo ya kuondoa muingiliano wa majukumu ya kiutendaji katika taasisi zinazohusiana na usimamizi wa biashara na majukumu ya mamlaka za udhibiti, kuwepo kwa utaratibu wa pamoja wa utoaji wa leseni,vibali na ada katika Biashara, Utalii, Uwekezaji na Usafirishaji.

"Aidha, inapendekeza kuanzisha mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya huduma mbali mbali zinazotolewa na taasisi zinazosimamia masuala ya biashara katika kutoa huduma na kutoa vibali vya kazi kwa wageni ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara.

"Natambua kwamba ili kuweza kuitekeleza Sera ya Biashara ya mwaka 2024 na Tathmini ya Mazingira ya Biashara ni lazima kila mdau apate fursa ya kuvisoma vitabu hivi ili kwa nafasi yake atimize wajibu wake ipasavyo.
"Napenda niwahakikishie kwamba Sera na Ripoti hii ilipita Serikalini na sisi tulipata fursa ya kuisoma na kuikubali.

"Hivyo basi kwa upande wetu kama Serikali, tutajitahidi kuyatekeleza na kuyasimamia yale yote yanayohusu upande wa Sekta ya Umma. Pia, niwaombe wadau kutoka Sekta Binafsi na washirika wa maendeleo tuendelee kushirikiana katika hatua zote za utekelezaji wa sera hii na kutekeleza mikakati maalum ya ukuzaji wa biashara kwa lengo la kukuza biashara hapa Zanzibar.

"Kama tulivyosikia juu ya tathmini ya mazingira ya ufanyaji biashara kwamba bado kuna changamoto katika urahisishaji biashara katika maeneo mbali mbali yakiwemo usafirishaji na uagiziaji bidhaa, usajili na uhaulishaji wa mali, upatikanaji wa vibali na mengineyo.

"Ahadi yangu ni kuwa Serikali itazifanyia kazi changamoto hizo na nazitaka Mamlaka za utoaji leseni na Mamlaka za usimamizi kuchukua hatua za haraka katika maeneo yote ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ili kurahisisha ufanyaji biashara na kuweza kufikia malengo ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050 na malengo ya Mpango wetu wa Maendeleo wa mwaka 2020/2021- 2025/2026."

Katika hatua nyingine,Rais Dkt.Mwinyi ameipongeza tena Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kwa mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha Sekta ya Biashara na Viwanda nchini.
"Ni faraja kubwa kwa Serikali kupata mafanikio makubwa na ya kujivunia katika kuendeleza Sekta ya Biashara. Ninaamini kuwa uzinduzi tunaoufanya leo utachangia kwa kiasi kikubwa katika ufanisi zaidi.
"Nitoe agizo kwa taasisi zote za Serikali kuitekeleza Sera na Ripoti ya Tathmini ipasavyo."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news