KINACHOMUANGUSHA Tundu Lissu leo ni genge la wanafiki waliomzunguka na kumdanganya kwa muda mrefu kuwa ana nguvu, ushawishi na uwezo wa kufanya yasiyowezekana.
Hili ndilo genge ambalo lilimweleza kuwa ana mamlaka ya kuzuia uchaguzi mkuu wa kikatiba kwa sababu tu yeye hajaridhika-jambo ambalo halina mantiki wala msingi wa kisheria.
Leo hii, haohao waliomshawishi kuwa ana uwezo wa kuzuia uchaguzi mkuu ndio haohao wametoweka kimya kimya, wakimuacha Lissu akihangaika peke yake kujibu tuhuma nzito za uhaini kwa kauli zake zisizokuwa na busara alizozitoa akidhani Watanzania watamfuata tu kila atakalosema-hata yale ya kijinga.
Tundu Lissu sasa anavuna alichopanda- matokeo ya kuzungukwa na wanafiki waliomwaminisha kuwa wako naye bega kwa bega hata pale anapovunja sheria.
Walimwaminisha kuwa Watanzania ni wajinga kiasi cha kutangazia nia ya kufanya uhaini na bado wakamshangilia. Amebaki peke yake; genge la wanafiki limemuacha solemba.
Lissu pia ameikaba koo Chadema. Chama chao sasa hakijui la kufanya wala pa kuanzia. Ni wao waliosema wazi kuwa "bila mabadiliko ya kisiasa hakuna uchaguzi" mwaka huu.
Ni wao hao waliokataa kutia saini fomu za maadili ya uchaguzi-sharti la kisheria linalotakiwa ili kushiriki uchaguzi mkuu.
Lakini sasa wanajitokeza kulalamika kwamba wamezuiwa kushiriki uchaguzi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Huu si unafiki wa wazi?
Baada ya mikakati ya hovyo na siasa za porojo kushindwa, viongozi wa Chadema sasa wanageukia wananchi-wakiwalaumu kwa “kutokuonyesha hasira” baada ya Lissu kukamatwa.
Ni jambo la kushangaza, hasa ikizingatiwa kuwa ni Lissu huyu huyu aliyewahi kumsanifu Freeman Mbowe na kusema kwamba akihamasisha maandamano anaishia kuandamana na binti yake tu.
Leo hii amekamatwa, na Watanzania wanaendelea na maisha yao kama kawaida. Hii ndiyo ishara kuwa Watanzania hawadanganyiki tena.
Hili ni fundisho kwa wanasiasa wanaotegemea mitandao ya kijamii kupanga siasa zao, wakishawishiwa na watu wasio na sura wala majina mitandaoni-ambao hata hawajitokezi barabarani bali hukaa kupost tu.
Ni wakati sasa kwa Lissu kupunguza siasa za mtandaoni na kuachana na ushauri wa wanaharakati walioko ughaibuni. Ashuke chini, atangamane na Watanzania wa kawaida walio hapa nchini.
Ukweli ni mmoja-si Tundu Lissu, si Chadema, wala wanaharakati wa ndani au nje ya nchi wenye uwezo wa kuzuia uchaguzi unaofanyika kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uchaguzi utafanyika mwaka huu, Watanzania watapiga kura, na wale wanaoona hawapo tayari kushiriki, wabaki pembeni bila kuvuruga haki ya wengine kutekeleza wajibu wao wa kiraia na kidemokrasia.
Kwa viongozi wa Chadema, huu ni wakati wa kufanya maamuzi ya msingi: Je, wanaamini kuwa bila wao hakuna uchaguzi? Kama jibu ni ndiyo, basi waache kuuhadaa umma na vyombo vya habari vya kimataifa kuwa wamezuiwa kushiriki.
Huwezi kuzuiwa kushiriki uchaguzi ambao wewe mwenyewe ulitangaza kuwa hautakuwapo kama matakwa yako hayatatimizwa.
Mwisho kabisa, nawaasa Watanzania waendelee kuwa waangalifu. Wakatae kuingizwa kwenye mitego ya kisiasa inayowekwa na watu wachache wenye ajenda binafsi.
Wasikubali kuvunja sheria kwa lengo la kutimiza tamaa za watu ambao maslahi yao binafsi ni muhimu zaidi kwao kuliko amani, utulivu na maendeleo ya nchi yetu.
Tags
Habari