ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameihakikishia Marekani kuwa, Zanzibar itaendesha uchaguzi kwa amani kwa ajili ya maendeleo na maanufaa ya nchi na wananchi.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipozungumza na Kaimu Balozi wa Marekani Tanzania,Andrew Lentz aliyefika Ikulu kujitambulisha.Amemuelezea Balozi huyo kuwa,Serikali inathamini kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) kwani imeleta Umoja,Amani na Mshikamano wa Wananchi wa Itikadi Tofauti za Kisiasa na kuifanya nchi kupiga hatua kubwa kwa maendeleo katika nyanja tofauti.
Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa,miaka mitano sasa nchi imebakia katika amani jambo ambalo Serikali inaendelea kuchukua kila juhudi kuhakikisha amani hiyo inakuwa ya kudumu wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.Akizungumzia masuala ya kiuchumi, Dkt.Mwinyi amesema,Zanzibar inathamini mchango unaotolewa na Serikali ya Marekani kwa Zanzibar hususani katika Sekta ya Afya,Elimu na Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi na Udhibiti wa Malaria.
Amesema,kwa kupitia misaada hiyo Zanzibar imefanikiwa vema kudhibiti malaria kwa kiwango kikubwa cha kupigiwa mfano na kusisitiza kuendelezwa kwa misaada hiyo.
Dkt.Mwinyi amesema, Zanzibar bado inahitaji kusaidiwa zaidi hasa katika kuimarisha uwekezaji katika Sekta za Kipaumbele za Uchumi wa Buluu na Utalii kwa misaada ya kifedha,kujenga uwezo wa kitaaluma kwa watendaji na mafunzo.
Aidha,amefahamisha kuwa nchi ina rasilimali nyingi za bahari ambazo zikifanyiwa kazi ipasavyo na kuwekeza hususani katika Sekta ya Uvuvi na Zao la Mwani zitainufaisha nchi kwa kiasi kikubwa.
Akizungumzia Sekta ya Utalii ameilezea kuwa, ni sekta muhimu inayochangia asilimia 30 ya pato la nchi ambayo inahitaji misaada zaidi na kuishauri Marekani kufikiria kuisaidia Zanzibar katika eneo hilo pamoja na kuzishauri sekta binafsi za pande zote mbili kushirikiana kuwekeza katika fursa mbalimbali ziliopo nchini.
Naye Kaimu Balozi Andrew Lentz ameihakikishia Zanzibar kuwa,nchi hiyo itaendeleza ushirikiano na Zanzibar uliopo kwa miaka mingi katika kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za Elimu,Afya na Utalii.
Akizungumzia masuala ya kisiasa ameishauri kuzingatiwa kwa fursa za mazungumzo na majadiliano ili kuyapatia ufumbuzi masuala ya kisiasa kwa amani na kufanya uchaguzi wa amani.






