DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. Marianne Young, katika ofisi za Benki Kuu jijini Dar es Salaam tarehe 29 Aprili 2025.

Katika mazungumzo hayo, Gavana Tutuba alieleza kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika licha ya changamoto mbalimbali za kiuchumi duniani.
Alibainisha kuwa kwa kipindi kinachoishia Desemba 2024, uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.5, hali inayoonesha ustahimilivu wa kiuchumi wa taifa.
Aidha, Gavana Tutuba alifafanua kuwa kuimarika kwa uchumi kumeambatana na kudhibitiwa kwa mfumuko wa bei, ambao ulikuwa asilimia 3.1 kufikia Desemba 2024.
Aliongeza kuwa sekta ya fedha nchini inaendelea kukua kwa kasi, huku Benki Kuu ikiimarisha juhudi za kuongeza huduma jumuishi za fedha kwa wananchi wote, ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanatumia mifumo rasmi ya fedha na kuchangia maendeleo ya taifa.
Alisisitiza kuwa Uingereza itaendelea kushirikiana na BoT katika masuala ya uchumi na fedha, sambamba na kukuza maendeleo endelevu ya Tanzania.