BoT yazitaka taasisi za fedha, wadau wa sekta ya madini kubuni mifumo bunifu ya kifedha

DAR-Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Yamungu Kayandabila, ametoa wito kwa taasisi za fedha na wadau wa sekta ya madini kubuni mifumo bunifu ya kifedha itakayowezesha wachimbaji wadogo na wa kati kupata mitaji kwa urahisi, ili kukuza sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa sekta ya madini uliofanyika tarehe 22 Mei 2025 katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, ulioandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Uuzaji wa Bidhaa Nje ya Afrika (Afreximbank) kwa kushirikiana na BoT, Dkt.Kayandabila, alisema kuwa licha ya dhahabu kuchangia zaidi ya asilimia 90 ya mauzo ya madini nje ya nchi, wachimbaji wadogo bado wanakabiliwa na changamoto kubwa za kifedha zinazowazuia kukuza shughuli zao.
“Changamoto hizi zinatokana na uendeshaji usio rasmi, ukosefu wa kumbukumbu za kifedha, pamoja na hatari kubwa za kijiolojia katika miradi ya uchimbaji. Hii huwafanya wawe wa hatari kwa taasisi za kifedha,” alisema Dkt. Kayandabila.

Alieleza kuwa taasisi nyingi za kifedha huona miradi ya wachimbaji wadogo kama miradi chipukizi isiyo na rekodi ya nyuma ya uendeshaji au nyaraka rasmi za kuaminika, hali inayosababisha hata miradi iliyokwisha kuanza na inayoonyesha mafanikio kushindwa kupata mikopo.
“Wengi wanashindwa pia kukidhi masharti ya dhamana au kufikia viwango vya uwazi wa taarifa vinavyotakiwa, jambo ambalo linawanyima fursa za kifedha,” aliongeza.
Dkt. Kayandabila aliipongeza Afreximbank kwa ubunifu wao wa kifedha, akisema taasisi hiyo ina nafasi muhimu ya kujaza pengo lililoachwa na benki za biashara kwa kutoa mikopo ya mradi, dhamana za mikopo, na mbinu mbadala za utoaji wa mitaji.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Mahusiano na Wateja wa Afreximbank, Bw. Eric Monchu Intong, alisisitiza dhamira ya benki hiyo katika kuiwezesha sekta ya madini kupitia mkakati wa njia mbili: kuboresha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya uchimbaji na kusaidia ujenzi wa uwezo wa ndani.
Alisisitiza umuhimu wa kuongeza thamani kabla ya kuuza madini nje ya nchi, kama vile uchenjuaji wa madini hapa nchini, akisema hatua hiyo itaongeza ajira, kupunguza umasikini, na kuleta manufaa ya kiuchumi ya kudumu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news