MOROGORO-Rais wa Zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki ametembelea eneo la kihistoria la Mazimbu, lililoko mkoani Morogoro ikiwa ni katika Maadhimisho ya Siku ya Afrika ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Mei.
Ziara hiyo maalum imebeba uzito mkubwa wa kihistoria na kiishara, ikikumbusha mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi kwa Afrika Kusini wakati wa mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo .Eneo la Mazimbu, kwa sasa ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), lilikuwa makazi na kituo cha mafunzo kwa wapigania uhuru wa Chama cha African National Congress (ANC) kilichokuwa kinaongozwa na Hayati Nelson Mandela.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Mbeki ametembelea makaburi ya wapigania uhuru waliofariki na kuzikwa katika eneo hilo na kuweka shada la maua, amepanda mti wa kumbukumbu na kutembelea hospitali ya SUA ambayo ilikuwa ikiwahudumia wana ANC hao katika eneo la Mazimbu na kuzungumza na uongozi wa SUA ulioongozwa na Mkuu wa Chuo hicho Mzee Joseph Warioba.Mheshimiwa Mbeki ameahidi kuwa Taasisi yake kwa kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere itaenda katika eneo hilo na kuandaa makala maalum ya picha Mwendo kwa lengo la kuhifadhi na kuipeleka historia ya eneo hilo kwa wananchi wa Afrika Kusini ili wauone mchango wa Tanzania kwao.
Akizungumza baada ya kuzuru Makaburi hayo Mheshimiwa Mbeki wa ametoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Tanzania na wananchi wake kwa uungwaji mkono usioyumba ambao walioutoa kwa ndugu zao wa Afrika Kusini wakati wa nyakati za dhiki.
“Mazimbu ni nyumbani kwetu, eneo hili si sehemu ya historia ya Afrika Kusini tu, bali ni alama ya mshikamano wa kweli wa Afrika. Tanzania ilisimama nasi wakati wa giza kuu la ukandamizaji. Leo tuko huru kwa sababu mlitupokea, mkatufundisha, na mkatupa hifadhi,” alisema Mbeki kwa hisia.
Taasisi ya Thabo Mbeki kwa Kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa pamoja wameshirikiana na kuandaa Maadhimisho ya Siku ya Afrika 2025 ambapo Mhadhara wa 15 wa Taasisi ya Thabo Mbeki utafanyika jijini Dar es Salaam tarehe 24 Mei ili kuadhimisha siku ya Afrika nchini.
Ziara hii ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Afrika, yanayoadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Mei, ikiwa ni kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika (zamani OAU) na kuhamasisha mshikamano, maendeleo na utambulisho wa bara la Afrika.
Mheshimiwa Mbeki yuko nchini pamoja na Taasisi ya Thabo Mbeki ambao wanashirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere na Chuo Kikuu cha Afrika Kusini kuadhimisha ya Siku ya Afrika mwaka 2025.Tarehe 25 Mei, 2025 Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Umoja wa Mabalozi wa Afrika (ADG) wameandaa mbio maalum zijulikanazo kama Afrika Day Marathon kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Afrika.
Mbio hizo za Kilomita 5, 10 na 21 zitaanzia katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere na kumalizikia hapo hapo.





