MOROGORO-Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kati, Devotha Mathew Minja ametangaza kujiuzulu nafasi zake zote ndani ya chama hicho na kujiondoa uanachama.

Minja amewaeleza wanahabari kuwa,hatua hiyo imefikiwa baada ya kutafakari kwa kina juu ya mustakabali wake kisiasa na kuona kuwa CHADEMA kimepoteza dira na lengo kuu la kisiasa ambalo ni kushika dola.
“Nimeamua kuondoka. Chama kimepoteza mwelekeo. Sasa ni wakati wa kutafuta mlango mwingine."
Kanda ya Kati inahusisha mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida ambako pia anatokea Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Tundu Lissu.
Minja ameeleza kuwa, kutoshiriki kwa chama hicho katika uchaguzi ni uamuzi wa watu wachache, ambao hauakisi nia ya wanachama walio tayari kupambana ili kushika dola.
“Msingi wa chama cha siasa ni kushika dola. Ukiacha kushiriki uchaguzi, hiyo dola utashikaje? Ndoto zetu za kuwatumikia wananchi haziwezi kufa kwa sababu ya misimamo ya watu wachache."