NA GODFREY NNKO
WANANCHI katika maeneo mbalimbali nchini wameonesha utayari wa kushiriki kwa nguvu zote katika udhibiti wa kilimo na matumizi ya bangi kuanzia ngazi za vitongoji.
Utayari huo unakuja baada ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) kwa nyakati tofauti kuendesha operesheni za mara kwa mara katika kanda mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kuhusu madhara ya kujihusisha na zao hilo haramu.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, sura ya 95, kilimo na biashara ya bangi hapa Tanzania ni kosa la jinai.
Hivyo, kujihusisha kwa namna yoyote na bangi kwa maana ya kulima, kuuza, kuhifadhi, kutumia, kuichakata au kwa namna nyingine ni kosa la jinai na adhabu yake inafikia hadi kifungo cha maisha jela.
Kwa nini bangi ni haramu?
Bangi ambayo ni dawa ya kulevya inayotokana na mmea unaoitwa Cannabis Sativa ambao hustawi na hutumika kwa wingi hapa nchini na duniani kote,huathiri ubongo na kubadili jinsi tunavyotafsiri uhalisia wa vitu.
Tafiti nyingi zimefanyika kuhusu bangi, na wataalamu wamebaini madhara mengi ya kiafya na kijamii kutokana na matumizi yake.
Aidha,tafiti zinaonesha kuwa, bangi huathiri uwezo wa kumbukumbu ya muda mfupi na uwezo wa kujifunza, hasa kwa watumiaji wa muda mrefu.

"Kwa wanafunzi na vijana matumizi ya bangi hupunguza uwezo wao wa kufikiri, kusoma na kukumbuka na hii hupelekea kupata matokeo yasiyoridhisha katika masomo yao."
Vilevile kuna uhusiano kati ya matumizi ya bangi na hatari kubwa ya matatizo ya akili kwani huamsha magonjwa ya akili hususani msongo wa mawazo,anxiety, psychosis na schizophrenia.
Pia,moshi wa bangi huzalisha lami na kemikali mbalimbali ambazo zinaweza kusababisha saratani ya mapafu na huathiri mifumo ya fahamu na kumfanya mtumiaji awe kwenye hali ya njozi ambapo ataona na kusikia vitu tofauti na uhalisia.
Hali hii inachangia kupunguza stamina ya mtumiaji na kusababisha ajali, uharibifu wa mali pamoja na kushusha ufanisi wa kazi.
Aidha,baadhi ya watumiaji hupata wasiwasi mkubwa mara wavutapo na kuwahisi vibaya watu wanaowazunguka kuwa wanataka kuwadhuru au kuhisi wanajua kuwa wamevuta bangi.
Wasiwasi huweza kumfanya mtumiaji amshambulie mtu na kumdhuru bila hatia.

Katika hatua nyingine,mtumiaji wa bangi hukosa mwamko wa maendeleo akijihisi ni mwenye maendeleo makubwa wakati anaishi maisha duni kabisa.
Mbali na hayo,matumizi ya bangi huchochea mmomonyoko wa maadili kutokana na ongezeko la vitendo vya uhalifu ikiwemo wizi, utapeli na ukatili wa kijinsia katika jamii.
Bangi husababisha utegemezi, huvuruga mahusiano ya kifamilia pamoja na upotevu wa ajira kwa mtumiaji.
Matokeo ya kuvurugika mahusiano ni pamoja na kuwepo kwa migogoro isiyoisha, kutelekeza wenza na watoto, kuvunjika kwa ndoa, kutokuwa na ajira, ongezeko la watoto wa mitaani na biashara ya ngono.
Msimamo wa Kamishna Jenerali Lyimo
Ili kuhakikisha Tanzania inabaki salama bila dawa za kulevya,Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas James Lyimo tangu awali aliweka wazi malengo yake katika kupambnana na dawa za kulevya nchini.
Aprili Mosi, 2023 Kamishna Jenerali Lyimo aliyaweka wazi malengo hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mtwara kwenye tukio la uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa.
Katika tukio hilo, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilishiriki kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
“Mimi kama kamishna mpya wa mamlaka hii, malengo yangu niliyoingia nayo ni kuhakikisha tunadhibiti kabisa uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini.
"Kwa hiyo nitoe wito kwa watumiaji wa dawa za kulevya kuacha kutumia dawa hizo, lakini pia wale wauzaji na wasambazaji wa dawa hizi kuacha kabisa biashara hiyo, kwani tunafanya operesheni kabambe nchi nzima, na tutahakikisha vijiwe vyote vya wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya vinasambaratishwa.
“Tutafafanya operesheni nchi nzima na tutawakamata wanaofanya biashara ya dawa kulevya.
"Lakini pia tutafanya operesheni kijiji kwa kijiji mikoa yote kuhakikisha kwamba wale wote wanaolima bangi na mirungi tunawakamata na kuteketeza mashamba yao.
"Kwa hiyo nitoe wito kwa wananchi, mashirika ya dini na serikali kwa ujumla kuhakikisha kwamba tunatoa taarifa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ili kuweza kufanikisha operesheni mbalimbali katika kudhibiti dawa za kulevya,”aliweka wazi Kamishna Jenerali Lyimo.
Vilevile, alitoa wito kwa jamii kutambua kuwa ushirikiano wao utaiwezesha nchi kuwa salama na huru bila dawa za kulevya, kwani dawa za kulevya zina madhara makubwa sana kijamii, kiafya, kimazingira na kiuchumi.
Wananchi waamua
Kutokana na elimu inayotolewa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), mwishoni mwa mwaka 2024 wananchi wa Kijiji cha Nkerege kilichopo Kata ya Kiore wilayani Tarime mkoani Mara waliamua kushirikiana na DCEA katika zoezi la kufyeka na kuteketeza mashamba ya bangi ili kuleta hali ya amani na utulivu kijijini hapo.

Uamuzi huo ulitokana na hofu iliyojitokeza wakati wa operesheni ya kuondoa bangi chini ya DCEA, ambapo watu walikimbia makazi yao wakihofia kukamatwa jambo lililoathiri shughuli zao za kijamii na kiuchumi.
Diwani wa Kata ya Kiore,Mheshimiwa Rhobi John anasema kwamba, wananchi wa Nkerege kwa kauli moja wameikataa bangi na kilimo hicho hakitalimwa tena kijijini hapo.
“Akina baba, akina mama na vijana wote wameamua bangi haitaonekana tena, yaani sisi wenyewe tutakuwa walinzi sisi kwa sisi.
"Unapoona mwenzako analima ni lazima kufuatilia na kutoa taarifa. Naishukuru cabinet ya wanasheria kutoka mamlaka kutoa elimu, akina mama na vijana walikuwa hawajapata elimu na walidhani hili ni zao bora kwao."
Naye Julius Zakaria Matiku, mwenyekiti wa mila katika ukoo wa Wasweta anasema, "Tumekubaliana kuteketeza bangi ili kuondoa tatizo hili la kukimbiakimbia.
"Kijana atakayekamatwa akilima bangi, nitalipiza faini ya ng'ombe watano,"amesema na kuongeza kuwa, mzee wa mila ana jukumu la kuhakikisha kuwa sheria zinaheshimiwa katika kijiji.
Kwa upande wake katibu wa mila, Burima Marwa Nyawise anasema kama wazee, wameamua kuteteketeza bangi ili waweze kulima mazao mengine kama mahindi, ufuta na kuendelea kufuga mifugo yao katika pori hilo.
"Pori hili ni safi kwa kulima kitu chochote kama vile mahindi maharage ufuta vinakubali. Kwa hiyo, hili zao la bangi limetutosha.
"Sasa watoto watulie nyumbani, wanawake wapikie watoto. Sisi malengo yetu ya kuja humu ni kuhakikisha tumeliteketeza hili zao la bangi."
Kamishna Jenerali Lyimo
Kupitia operesheni hiyo, ambayo Mamlaka ya Kudhiitia Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) inaendelea kufanya nchi nzima ili kuhakikisha dawa za kulevya za mashambani na viwandani zinatokomea na Tanzania inakuwa huru dhidi ya dawa za kulevya, Kamishna Jenerali Lyimo amesema kuwa,kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wamefanya operesheni hiyo katika vijiji vya Matongo, Nyarwana na Weigita vilivyopo Bonde la Masinki.
Sambamba na vijiji vya Nkerege, Kembwe, Nyakunguru na Iseresere na eneo la Bonde la Mto Mara.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo ambaye aliongoza operesheni hiyo mwishoni mwa mwaka jana amesema, jumla ya ekari 3,007.5 za mashamba ya bangi zimeteketezwa katika operesheni hiyo.
Aidha, kilogramu 7,832.5 za bangi kavu, na kilogramu 452 za mbegu za bangi zilikamatwa, ambapo watuhumiwa 17 walikamatwa na tayari wamefikishwa mahakamani.
Kamishna Lyimo amesema,operesheni hii ni sehemu ya jitihada za serikali kulinda jamii dhidi ya madhara ya dawa za kulevya na amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kutoka kwa wananchi katika kutoa taarifa kuhusu shughuli zinazohusiana na dawa hizo.

Amesema,mamlaka imebaini kuwa, kilimo cha bangi mkoani Mara kinafadhiliwa na raia wa nchi jirani ambao huwapa mitaji wakulima wa Tarime kisha bangi ikishakomaa huvunwa na kusafirishwa kwenda kuuzwa.
“Tutafanya operesheni kubwa kwa namnna nyingine na kuhakikisha maeneo haya yanabadilishiwa matumizi na hayatumiki tena kwa kilimo cha bangi. Pia wote wanaotetea uhalifu huu watachukuliwa hatua ili kuhakikisha wanachi wote wanatii sheria za nchi.”
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mheshimiwa Meja Edward Gowele amekiri wilaya yake inakabiliwa na changamoto ya kilimo cha bangi hususani katika eneo la Bonde la Mto Mara na tayari Serikali imeanza kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na changamoto hiyo.
Amesema,tayari wameanza kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya bangi na hasara wanayoweza kuipata kwa kujihusisha na kilimo cha bangi na walio wengi wameahidi kuachana na kilimo cha bangi.
Mwita Mataro ambaye ni Afisa wa Maji kutoka Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria dakio la Mara ambaye pia ni msimamizi wa rasilimali za maji katika Mkoa wa Mara amesema,amejionea hali halisi ya bonde na ameshuhudia zao la bangi likiwa limelimwa katika Bonde la Mto Mara.

"Sheria za rasilimali za maji haziruhusu kilimo haramu cha zao la bangi. Hata mazao mengine halali yanapaswa kulimwa umbali wa mita 60 kutoka mtoni.
"Hao wanaolima bangi ni sehemu ya watu wanaoharibu vyanzo vya maji kwa sababu mwisho wa siku huu udongo wote mvua zitakaponyesha tope lote linatiririka kwenda kwenye mto.’’
Mataro ameongeza kuwa,bodi hiyo imeandaa mpango kwa kidakio cha Kaskazini ambao unataja shughuli gani zinatakiwa kufanyika kwenye vyanzo vya maji ambazo ni rafiki, na wao kama bodi watasimamia kuhakikisha mipango hiyo inatekelezwa na hifadhi ya maji inalindwa.
Kwa upande wake Lepapa Molel ambaye ni Afisa Kilimo kutoka ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Mara amesema,wakulima wengi wanalima bangi kwa kutegemea maji yanayotoka Mto Mara.
“Nashauri wakulima wageuke na kuanza kulima mazao ya chakula yanayoweza kuwapa chakula na fedha kuliko bangi”.
Kondoa
Operesheni hizi na elimu inayotolewa na DCEA kwa wananchi imeendelea kuwa na matokeo mazuri.
Kwani, hivi karibuni wananchi wa Kata ya Haubi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma walishirikiana na mamlaka na vikiwemo vyombo vingine katika kutokomeza kilimo haramu cha bangi katika maeneo ya Hifadhi ya Milima ya Haubi.
Kwa mujibu wa DCEA, operesheni hii ni ya pili kufanyika mwaka huu katika Wilaya ya Kondoa ambapo Januari walibaini na kuteketeza zaidi ya ekari 500 za bangi.
DCEA imebainisha kuwa,kupungua kwa mashamba hayo hadi ekari 157 ni ushahidi kuwa wananchi wameanza kuelewa na kushiriki kikamilifu katika jitihada hizi muhimu.
DC
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Mhe. Fatuma Nyangasa amesisitiza kuwa,serikali ya wilaya itaendelea kushirikiana kwa karibu na DCEA katika kuhakikisha kilimo cha bangi kinatokomezwa kabisa na kusisitiza kuwa elimu kwa wananchi itaendelea kutolewa.
Amesema,lengo ni ili waachane na kilimo hicho haramu na badala yake wajikite katika uzalishaji wa mazao halali ya chakula na biashara kama vile tumbaku, ufuta na maharage.
“Tunawaomba wananchi waachane na kilimo haramu cha bangi. Serikali ipo tayari kuwaongoza katika kuelekea kilimo halali na chenye tija. Ushirikiano baina ya serikali na wananchi ndiyo silaha kubwa ya kuikomboa jamii yetu."
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mafai, Shaibu Hamis Kalinga ameweka bayana kuwa kijijini hapo kumekuwa na historia ya kilimo cha bangi kwa muda ndefu, lakini kwa sasa viongozi wa kijiji wamejipanga kuongoza mapambano dhidi ya zao hilo haramu.
“Zamani bangi ilikuwa kama sehemu ya maisha kwa baadhi ya wakulima hapa kijijini, lakini sasa tunaelewa madhara yake. Tumejipanga kutoa elimu na kuhamasisha kilimo halali tu," alisema Kalinga.
Rajabu Hamis ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mafai amepongeza juhudi za serikali kwa kutoa elimu kwa Wananchi jambo ambalo limebadili fikra za wananchi kuhusu bangi.
“Tulilima bangi kwa sababu ya kukosa njia mbadala, lakini baada ya kupewa elimu na kuona jitihada za Serikali, tumeamua kuachana na bangi na kushirikiana na mamlaka kuitokomeza kabisa."
Operesheni na elimu dhidi ya dawa za kulevya imeendelea kutolewa na DCEA ikiwa taarifa ya hali ya dawa za kulevya ya mwaka 2022 inaonesha kuwa, mikoa ya Arusha, Manyara, Iringa, Morogoro,Manyara, Ruvuma na Mara inaongoza kwa kilimo cha bangi.
Pongezi
Kwa nyakati tofauti wananchi wa Keko na Chamanzi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam wamepongeza Kamishna Jenerali Lyimo kwa uongozi thabiti ambao umekuwa wa vitendo zaidi katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
"Vijiwe vingi vya wavuta bangi huku Keko vimesambaratika kwa sababu, kwanza upatikanaji wake kutoka shamba ni mgumu,"anasema Ibrahim Said mkazi wa Keko Magurumbazi huku akiongeza kuwa sababu kuu inatokana na udhibiti uliofanywa na DCEA.
Amesema, baada ya Kamishna Jenerali Lyimo kuonekana katika mitandao ya kijamii akishirikiana na wananchi kufyeka mashamba makubwa ya bangi huko mikoani waliokuwa wanajihusisha na uuzaji wengi wameacha na wameama katika mji huo.
Zulfa Omary mkazi wa Chamanzi anasema,kazi inayofanywa na DCEA kutokomeza bangi ni nzuri na inafaa kuungwa mkono.
"Bangi ni chanzo cha wengi kujiingiza katika ututaji wa unga (heroin), hivyo nimpongeze sana Kamishna Jenerali Lyimo kwa kazi nzuri anayofanya kudhiti dawa zote za kulevya, anafanya kazi nzuri,Mwenyezi Mungu ndiye atakayemlipa kwa wema wake kwa Watanzania. Dawa za kulevya ni hatari sana, usiombe ndugu yako aingie katika huo mkumbo,"amesema Zulfa Omary katika mahojiano na DIRAMAKINI.