Iringa Mkwawa Rally kupaisha utalii

IRINGA-Benki ya Taifa ya Biashara (NBC Bank) imedhamiria kuyatumia mashindano ya mbio za magari ya Iringa Mkwawa Rally ili kutangaza na kuimarisha sekta ya utalii katika mkoa huo unaosifika kwa utalii wa kiutamaduni na vivutio mbalimbali vya asili.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Idara ya Bidhaa na Mauzo wa benki hiyo, Abel Kaseko, katika hafla fupi ya kuhitimisha mashindano hayo msimu wa mwaka 2025, yaliyofanyika kwa siku mbili mkoani Iringa huku mshiriki Bird Manveer akiibuka mshindi.

"Tumejizatiti kutumia jukwaa hili kuonesha vivutio vingi vya utalii vilivyopo katika eneo hili, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo ndiyo hifadhi kubwa zaidi nchini Tanzania pamoja na vivutio vingine vingi vya kihistoria na kiutamaduni," Kaseko amefafanua.

Kaseko amefichua kwamba benki hiyo sasa itaangazia pia michezo kama mbio za magari, golf, na masumbwi kama michezo ya ziada baada ya kuwekeza zaidi kwenye soka na marathon.

Akifunga mashindano hayo ambayo hufanyika kila mwaka, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James, ameipongeza Benki ya NBC na wadau wote waliohusika katika kufanikisha tukio hilo akisema;-

"Kupitia mashindano haya, tumeweza kuonesha na kuuza bidhaa na huduma tofauti kuanzia malazi hadi vyakula vya jadi na hivyo kufanikisha ukuaji wa utalii katika eneo hili."

Naye mshindi wa mashindano, Bird Manveer, amepongeza jitihada za waandaaji na Benki ya NBC akisema “Kushiriki na madereva wengine wenye uwezo mkubwa hakika kumetupatia changamoto sana, na nimefurahia changamoto hiyo."

Kwa upande wake msimamizi wa mashindano hayo, Hidaya Kamanga amesema madereva wengi bado wanakumbana na changamoto za kupata udhamini, hivyo kuathiri ushiriki wao katika matukio hayo ya kusisimua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news