NA LWAGA MWAMBANDE
MEI 20,2025 Wizara ya Afya ilieleza kuwa, tangu mwezi Februari hadi Aprili,mwaka huu kumekuwepo na ongezeko la visa vya UVIKO-19 kutoka asilimia 1.4 (wagonjwa 2 kati ya watu 139 waliopimwa) mwezi Februari hadi asilimia 16.3 (wagonjwa 31 kati ya 190 waliopimwa) mwezi Machi, na kisha asilimia 16.8 (wagonjwa 31 kati ya watu 185 waliopimwa) mwezi Aprili 2025.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali ilieleza kuwa,kuongezeka na kupungua kwa UVIKO -19 kumekuwepo kila mwaka tangu kutangazwa kwa ugonjwa huo mwaka 2020.
Aidha, wizara imebainisha kuwa,ongezeko hilo linaonekana zaidi katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mshairi wa kisasa,Lwaga Mwambande licha ya licha ya kukumbushia mambo muhimu kuhusu UVIKO-19, pia ameendelea kusisitiza lila mmoja kuchukua tahadhari. Endelea;
Watu kadha wanagonjwa, ndivyo tulivyoambiwa,
Sisi tusio wagonjwa, hili vema kuelewa,
UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.
²Wapo wanasimulia, ya kwamba wamepitiwa,
Asante wamesalia, tupate kusimuliwa,
Wengine wameishia, twasema wametwaliwa,
UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.
³Zamu hii inatisha, jinsi tunafanyiziwa,
Inavamia maisha, bila ya kujielewa,
Mara pumzi yaisha, uhai wakatiliwa,
UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.
⁴Kazi sasa kujikinga, tusije tukafikiwa,
Piga chafya domo kinga, mate tusijefikiwa,
Hiyo kwetu njema kinga, bora kama twaelewa,
UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.
⁵Vitu vya maambukizi, siyo vya kusogelewa,
Ukishika hivyo wazi, waweza ukafikiwa,
Uwasake wauguzi, wakati unapaliwa,
UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.
⁶Kama mtu anaumwa, UVIKO hujaelewa,
Na akili ukatumwa, apate kusogelewa,
Nawe waweza kuumwa, hili vema kuelewa,
UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.
⁷Tahadhari ni muhimu, kama mtu ahisiwa,
Pale ukimhudumu, hakika kuielewa,
Hapo waweza kudumu, usijeukavamiwa,
UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.
⁸Dalili ugonjwa huu, homa kali kupitiwa,
Kikohozi juujuu, kikavu unafikiwa,
Kupumua muda huu, shida unaingiliwa,
UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.
⁹Chakula unakipenda, ladha unapotelewa,
Koo kichwa vinadunda, maumivu wazidiwa,
Hapo sipitali nenda, kwa vipimo kufanyiwa,
UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.
¹⁰Kujikinga na kadhia, mikono sabuni nawa,
Na vitakasa tumia, hivi unanielewa,
Kitumia hizi nia, huwezi ukafikiwa,
UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.
¹¹Wakati unakohoa, kujifunika elewa,
Chafya uzijekutoa, wengine wakavamiwa,
Hivyo vaa barakoa, pale inahitajiwa,
UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.
¹²Epuka mikusanyiko, isiyo lazima sawa,
Na UVIKO chanjo iko, ni vema ukapatiwa,
Hapo usalama wako, vema utaangaliwa,
UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.
¹³Tambua hakuna tiba, UVIKO ukijiliwa,
Ni dalili kuzikaba, tatizo kudhibitiwa,
Tahadhari zote beba, na ziweze kutumiwa,
UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.
¹⁴Na tulio wa imani, Mungu tunaomwelewa,
Vema kwenda magotini, tuombe tutasikiwa,
Kwamba tusiwe shidani, UVIKO tukazidiwa,
UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
