DAR-Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amejiuzulu rasmi nafasi ya Urais wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ili kuelekeza nguvu kwenye majukumu yake mapya ndani ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Karia ameacha kiti hicho muda mfupi baada ya kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF.
Katika kipindi chake akiwa CECAFA, Karia alifanikiwa kuiinua kanda hiyo na kuifanya kuwa miongoni mwa bora ndani ya CAF, kwa maboresho makubwa ya mashindano na uongozi.
TFF imempongeza Karia kwa mafanikio hayo na mchango wake mkubwa katika kuleta heshima kwa taifa kupitia nyanja za kimataifa za soka.