DAR-Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza kuanza kwa mitihani ya kuhitimu kidato cha sita na Ualimu ngazi ya Cheti na Stashahada, inayotarajiwa kuanza kesho Mei 5, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa NECTA Dkt. Said Mohamed amesema watahiniwa 134,390 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha sita na watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani wa ualimu ni 10,895.
Dkt.Mohamed ametoa wito kwa watahiniwa, wasimamizi, wakuu wa shule na wamiliki wa shule na vyuo nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa ili kuhakikisha mitihani hiyo inafanyika kama ilivyopangwa.
Ameongeza kuwa, NECTA tayari limekamilisha maandalizi yote ikiwa ni pamoja na kusambaza mitihani na nyaraka zote muhimu katika maeneo yote ili kufanikisha kufanyika kwa mitihani hiyo.
