DAR-Mshambuliaji wa timu ya Dodoma Jiji, Iddi Kipwagile amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Aprili wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2024/25, huku Miloud Hamdi wa Yanga, akichaguliwa kuwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.
Kipwagile alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiwashinda Pacome Zouzoua wa Yanga na Haruni Chanongo wa Tanzania Prisons, alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo minne ambayo Dodoma Jiji ilicheza mwezi huo na kufunga mabao matatu na kuhusika na mengine matatu kwa dakika 320 alizocheza.
Kwa upande wa Hamdi aliyeingia fainali na Amani Josiah wa Tanzania Prisons na David Ouma wa Singida Black Stars, aliiongoza Yanga kushinda michezo yote minne iliyocheza mwezi huo na kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi Kuu ya NBC. Yanga ilizifunga Tabora United (0-3), Coastal Union (1-0), Azam (1-2) na Fountain Gate (0-4).
Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Isamuhyo uliopo Dar es Salaam, Ashraf Omar kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Aprili kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.
Wakati huohuo Kamati ya Tuzo za TFF, imemchagua Emmanuel Maziku wa Stand United kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Aprili wa Ligi ya NBC Championship 2024/25, huku Ramadhan Ahmada wa Transit Camp akichaguliwa kuwa Kocha Bora wa mwezi huo.
Maziku aliyeingia fainali na Mohammed Hassan wa Transit Camp na Ramadhan Kipalamoto wa Songea United, alionesha kiwango chenye mwendelezo, ikiwa ni pamoja na kufunga mabao manne kwa dakika 194 alizocheza kwenye michezo mitatu.
Kwa upande wa Ahmada aliyeingia fainali na Malale Hamsini wa Mbeya City na Awadh Juma wa Mtibwa, aliiongoza timu yake kushinda michezo yote mitatu iliyocheza na kupanda kutoka nafasi ya 15 hadi ya 13 kwenye msimamo wa ligi hiyo.