DAR-Mwanzilishi na Afisa Mtendaji Mkuu wa WazoHuru Media Group Limited Ndg Mathias Canal ameshinda Tuzo mbili za SAMIA KALAMU AWARDS sekta ya Ujenzi na chombo bora cha mtandaoni.

Tuzo hizo zimetolewa Mei 5,2025 katika ukumbi wa Super Dome Masaki Jijini Dar es salaam ambapo mgeni rasmi katika tukio hilo alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Tuzo hizo zimetolewa kwa wanahabari watanzania kwa lengo la kuhamasisha, kuhimiza na kukuza wigo wa uchakataji, utangazaji na uchapishaji wa maudhui ya ndani kupitia vyombo vya habari.
Tuzo hizi zitahusisha maudhui yaliyochapishwa kupitia magazeti, redio, televisheni, majukwaa ya mtandaoni pamoja na tuzo kwenda kwa vyombo vya habari. Tuzo hizi zinahusisha habari zilizochapishwa kati ya Januari 01 hadi Oktoba 26, 2024.

Aidha, utoaji wa tuzo hizi umelenga kuchochea uandishi wa makala zilizofanyiwa utafiti na uchambuzi kuhusu maendeleo ya nchi, uwajibikaji, uzalendo na kujenga chapa na taswira ya nchi.