Msajili asitisha kutoa ruzuku kwa CHADEMA

DAR-Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania ametangaza kusitisha kutoa ruzuku kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hadi pale watakapotekeleza maelekezo ya Ofisi ya Msajili, kutokana na Chadema kutokuwa na viongozi wanaoweza kusimamia mapato, matumizi na marejesho ya fedha hizo za umma.
Taarifa ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyotolewa Mei 27, 2025, na kusainiwa na Abuu Kimario, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Elimu ya Uraia imesema kuwa, kulingana na mamlaka aliyonayo chini ya Kifungu cha 18(6) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, hatua hiyo imechukuliwa baada ya Chadema kukaidi mara kadhaa maamuzi ya Ofisi ya Msajili, ikiwemo taarifa ya Mei 25, 2025.

Katika taarifa hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche, akisoma maazimio ya Kamati Kuu ya Chama, alieleza kuwa maamuzi na maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu malalamiko ya Bw. Lembrus Mchome ni batili na hawatayafanyia kazi.

Aidha, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeendelea kusisitiza kuwa Bw. John Mnyika, Amani Golugwa, Ali Ibrahim Juma, Godbless Lema, Dkt. Rugemeleza Nshala, Rose Mayemba, Salima Kasanzu, na Hafidhi Ali Salehe siyo viongozi halali wa Chadema, sambamba na watendaji wengine wote walioteuliwa katika kikao cha Baraza Kuu la Januari,2025.

Ofisi hiyo imewasihi wananchi, wadau, na mamlaka au taasisi za serikali na binafsi kutowapa ushirikiano au huduma wanachama walioorodheshwa hapo juu endapo watakuwa wakihitaji huduma fulani kama viongozi wa Chadema.

Imeeleza kuwa viongozi halali wa vyama vya siasa ni wale tu wanaotambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Msajili pia amebainisha kwamba endapo Chadema wataendelea kukaidi kutekeleza maamuzi na maelekezo waliyopatiwa, basi mamlaka husika zitatakiwa kuchukua hatua za kisheria na kijinai, pamoja na kuwasimamisha wanaojifanya kuwa viongozi wa Chadema katika kufanya shughuli za kisiasa kwa mujibu wa Kifungu cha 21E cha Sheria ya Vyama vya Siasa nchini.

Aidha, Msajili amekumbusha kwamba kwa mujibu wa sheria, anayo mamlaka ya kusimamisha usajili wa Chadema endapo kitaendelea kuwatambua wanaojiita viongozi wa chama hicho.

Ametaka vyama vya siasa kuheshimu sheria ili kuepuka migogoro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news