Msajili atengua uteuzi wa viongozi wa CHADEMA

DAR-Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ametengua uteuzi wa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Viongozi waliotenguliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa ni John Mnyika-Katibu Mkuu, Amani Golugwa - Naibu Katibu Mkuu (Bara) na Ally Ibrahim Juma-Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar).

Wengine ni Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk Rugemeleza Nshala (Mwanasheria Mkuu wa chama) Wajumbe wa Kamati Kuu ya Siasa ya Chadema.

CHADEMA imeagizwa iitishe tena kikao cha Baraza Kuu jipya na lenye akidi stahiki ambapo Msajili wa Vyama ameandika barua kutokana na malalamiko yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Lambrus Mchome.

Msajili ametoa maelekezo kwa CHADEMA kuitisha Baraza Kuu jipya lenye akidi stahiki, ili kufanikisha uteuzi upya wa viongozi hao kwa mujibu wa Katiba ya chama, Sheria ya Vyama vya Siasa, na kanuni zinazohusika.

Katika mafunzo ya viongozi wa BAWACHA na BAVICHA Kanda ya Kusini mnamo Machi 25, 2025, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alieleza kuwa akidi ya kikao hicho ilikuwa sahihi, kwa kuwa kilihusiana na uteuzi wa kawaida si mabadiliko ya katiba wala uchaguzi.

Mnyika alisema kikao hicho kilikuwa na zaidi ya asilimia 50 ya wajumbe, akisisitiza kuwa hiyo ilikuwa akidi ya kutosha kwa mujibu wa taratibu za ndani.

Hata hivyo, Ofisi ya Msajili, baada ya kupitia malalamiko ya Mchome na majibu ya CHADEMA, imeafiki kwamba akidi haikufikiwa na hivyo uamuzi wa kikao hicho si halali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news