NA GODFREY NNKO
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amefunga rasmi Kongamano la 18 la Kimataifa na Maonesho kuhusu Elimu ya Kidijitali, Mafunzo na Ukuzaji wa Ujuzi (eLearning Africa).
Kongamano hilo ambalo lilianza Mei 7,2025 lilifunguliwa Mei 8,2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es likiwa ni la pili kufanyika hapa nchini tangu liasisiwe mwaka 2005.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Hemed Suleiman Abdulla ambaye amemwakilisha Rais Dkt.Mwinyi katika ufungaji wa kongamano hilo Mei 9,2025 jijini Dar es Salaam akizungumza na viongozi mbalimbali na wataalamu wa kada ya elimu barani Afrika amesema, limekuwa ni kongamano lenye mafanikio makubwa.
Aidha,kongamano hilo limeongozwa na kauli mbiu isemayo Kufikiri upya elimu na maendeleo ya rasilimali watu kwa ustawi wa baadae wa Afrika.
"Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunajisikia fahari kubwa kuwa wenyeji wenu, ni imani yangu kuwa mmefarijika kuwa katika jiji la Dar es Salaam na mnapata na mnaendelea kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa Watanzania ambao ukarimu ndiyo msingi wao wa maisha."
Pia, ameipongeza Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na wadau wengine ambao wamefanikisha kongamano hilo kwa ubora wa hali ya juu.
Vilevile, amezipongeza kamati zote za maandalizi ikiwemo ile ya Kitaifa kwa jitihada zao ambazo zimewezesha kongamano hilo muhimu katika sekta ya elimu barani Afrika.
Amesema, ni jambo la faraja kuona washiriki ambao wameonesha bidhaa na huduma zao ambazo ni muhimu kwa kuleta masuluhisho ya changamoto mbalimbali ambazo jamii inakabiliana nazo katika kufikia viwango bora vya elimu.
Amesisitiza kuwa, bunifu zinazohusiana na teknolojia ni nguzo muhimu katika kuwezesha ufundishaji na kujifunza.
Amesema, Afrika ina nafasi kubwa zaidi ya kusonga mbele kiuchumi kutokana na wingi wa rasilimali za asili zilizopo kila kona ya bara hilo.
Kwa msingi huo, amewahimiza wataalamu wa bunifu kuona ni namna gani wanainua teknolojia jumuishi na shirikishi ambazo zitawasaidia Waafrika kuzitumia katika kuainisha zilipo rasilimali husika na kuziendeleza.
"Kupitia masuluhisho ya teknolojia za kisasa yatawezesha uendelezaji wa rasilimali zetu Afrika kwa ustawi wa uchumi na uendelevu wa miradi ya maendeleo."
Amesema, katika siku tatu za kongamano hilo ambalo limewakutanisha mamia ya wataalamu kutoka ndani na nje ya Tanzania limewapa fursa ya kushirikishana, kuchambua na kujadili mada mbalimbali.
Miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika kongamano hilo ni namna gani sekta ya elimu barani Afrika itakuwa jumuishi kwa makundi mbalimbali ya watu.
Nyingine ni mafunzo ya matumizi ya teknolojia za kidigitali kwa walimu, ushirikiano katika masuala ya teknolojia, matumizi ya Akili Unde (AI) katika sekta ya elimu ili kuwajengea Waafrika ujuzi wa teknolojia za kidigitali pamoja na kuwatengenezea fursa za ajira na uwezeshaji zaidi.
Makamu wa Pili wa Rais amesema kuwa,kupitia mijadala, elimu iliyotolewa katika maonesho ambayo ilikuwa jumuishi kwa wadau wote itaongeza hamasa ya kuimarisha na kukuza sekta ya elimu Afrika.
Licha ya kuwaomba washiriki wa kongamano hilo kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo bara na visiwani, pia Mheshimiwa Abdulla amewakaribisha wawekezaji kuwekeza Tanzania.
Amesema kuwa, Tanzania imepiga hatua kubwa katika uimarishaji wa miundombinu mbalimbali ambayo ni rafiki kwa wawekezaji, seta katika kila sekta hivyo milango ipo wazi kwao kuja kuwekeza ikiwemo upande Sayansi na Teknolojia.
Awali,Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa,kongamano hilo limefanyika kwa siku tatu hapa nchini kuanzia Mei 7 hadi 9,2025.
Prof. Mkenda amesema, kupitia kongamano hilo washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania waliangazia kwa kina fursa zilizopo katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Dhamira ikiwa ni kuzitumia ili ziweze kuchochea kasi ya ukuaji wa sekta nyingine ikiwemo ya elimu na namna ya kukabiliana na changamoto ambazo zinaambatana na ukuaji wa teknolojia hususani upande wa matumizi ya Akili Unde (AI).
Pia, amesema kongamano hilo limetoa mwongozo wa namna ambavyo elimu barani Afrika inapaswa kuwasilishwa kwa kutumia nyenzo muhimu za kidigitali.
Kwa upande wake Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema, Serikali ya Tanzania inatekeleza mpango wa miaka 10 wa mfumo wa uchumi wa kidijiti (digital economy).
Amesema, mpango huo ulizinduliwa Julai,2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Waziri Slaa amesema, hilo ni eneo muhimu katika kutekeleza Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 inayosisitiza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika sekta zote ili kuleta mapinduzi ya teknolojia na maendeleo.
Vilevile amesema, katika kufanikisha hayo Serikali imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya
kusambaza intaneti kupitia mifumo ya kisasa kote nchini.
Likiwa na dhamira ya kuimarisha elimu ya kisasa, kongamano hilo ambalo limefanyika kwa siku tatu limewakutanisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Pia, awali mawaziri mbalimbali kutoka barani Afrika walishiriki kikao maalumu (Ministerial Roundtable).
Dhamira ikiwa ni kujadili mikakati mbalimbali ikiwemo kuandaa rasilimali watu yenye maarifa na ujuzi pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika sekta mbalimbali hususani elimu barani Afrika.