DAR-Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Daniel Chapo, amewasili nchini kwa ziara ya Kitaifa ya siku tatu kuanzia tarehe 7 hadi 9 Mei, 2025 kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Rais Chapo atapokelewa rasmi Ikulu jijini Dar es Salam na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 08 Mei, 2025 na atakuwa na mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, atashuhudia uwekaji saini Mikataba na Hati za Makubaliano (MOU) katika sekta mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji, atatembelea Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika na Stesheni ya Reli ya Kisasa (SGR) jijini Dar es Salaam ili kujifunza na kuangalia fursa za ushirikiano.
Mheshimiwa Rais Chapo pia atatembelea visiwa vya Zanzibar ambapo atakuwa na mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt Hussein Ali Mwinyi, atatembelea miradi mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu na Soko la Samaki la Malindi.