Serikali yataja umuhimu wa Zanzibar CEOs Forum

ZANZIBAR-Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah amesema kuwa, Jukwaa la Wakuu wa Taasisi za Umma ni muhimu katika kujadili changamoto na mafanikio ya taasisi za serikali kwa lengo la kuchochea maendeleo ya taifa.
Hayo yamesemwa leo Mei 11,2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Sharif Ali Sharif, wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Kwanza la Wakuu wa Taasisi, uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Mhe. Sharif amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimejenga misingi imara ya utendaji ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Aidha, ameeleza kuwa Jukwaa hilo ni la kihistoria kwani kwa mara ya kwanza linafanyika Zanzibar, na ni hatua muhimu ya kutekeleza maono ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya kuwahimiza viongozi kuwa wabunifu katika taasisi wanazoziongoza ili kufikia malengo ya maendeleo.

“Jukwaa hili ni chachu ya mashirikiano, mshikamano na ubunifu baina ya viongozi wa taasisi, jambo litakalosaidia kuibua fursa mpya za maendeleo kwa taifa,” amesema Mhe. Sharif.
Amesisitiza kuwa ni vyema Jukwaa hilo likawa endelevu kila mwaka, ili kuwapa fursa wakuu wa taasisi kukutana, kubadilishana uzoefu, kufanya tathmini ya utendaji, na kuweka maazimio ya pamoja yatakayowezesha kuongeza ufanisi katika taasisi.

Viongozi wote walihimizwa kutumia fursa hiyo ipasavyo ili watakaporejea katika taasisi zao, waweze kuleta mabadiliko chanya ya kiutendaji yatakayowezesha utoaji bora wa huduma kwa wananchi.

Ameongeza kuwa ni lazima viongozi hao wazingatie misingi ya utawala bora katika ngazi zote, ikiwa ni pamoja na kufuata sheria, kuwa waadilifu, kuendesha shughuli kwa uwazi na kuwajibika, ili kuepuka changamoto kama vile ubadhirifu, rushwa na unyanyasaji.

Katika maelezo yake, Mhe. Sharif pia aliwataka wakuu wa taasisi kushiriki katika uchaguzi kwa amani ifikapo Oktoba 2025, na kuwahimiza wananchi kudumisha amani na utulivu – msingi wa maendeleo endelevu.

Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, alisisitiza umuhimu wa jukwaa hilo kutimiza dhima yake ya kuwa chombo cha viongozi kukumbushana majukumu yao, kuwa waaminifu, na wabunifu – sambamba na maelekezo ya viongozi wakuu wa nchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Bw. Juma Burhani, alisema lengo kuu la Jukwaa ni kuibua fursa za kibiashara na maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania Bara, kuchochea uchumi shirikishi na kuimarisha umoja wa kitaifa.
Aliongeza kuwa tathmini ya taasisi za umma itafanyika, na kwamba jukwaa hilo litakuwa endelevu kila mwaka ili kuongeza uwajibikaji na ubunifu.

Naye Msajili wa Hazina Zanzibar, Bw. Waheed Ibrahim Mohamed Sanya, alieleza kuwa maazimio yatakayopatikana kupitia Jukwaa hilo yataboresha utekelezaji wa majukumu ya taasisi na kuongeza tija katika maendeleo ya nchi.

Jukwaa hilo la siku tatu limewaleta pamoja wakuu wa taasisi za umma na binafsi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, chini ya kaulimbiu: “Uongozi Bunifu na Mashirikiano ni Muhimu ili Kufikia Maendeleo Endelevu Zanzibar.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news