NA GODFREY NNKO
MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umesema,Serikali imedhamiria kujenga uchumi wa kidijitali ndiyo maana wamejikita kupeleka na kufanikisha huduma ya mawasiliano kwa wananchi wote nchini.
Hayo yamesemwa leo Mei 26,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo,Mhandisi Peter Mwasalyanda katika kikao kazi na wahariri na waandishi wa habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) jijini Dar es Salaam.
Lengo la kikao kazi hicho ni mfuko kuelezea kazi kubwa ambazo wamefanya hususani katika kipindi hiki cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Amesema, mikakati ya mfuko ni kuona Watanzania wote bila kujali wanaishi mijini au vijijini wanafurahia huduma za mawasiliano kidijitali ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.
"Mawasiliano ni sawa na maji, ni sawa na umeme. Kwenye uchumi wa kidijitali tunataka kila mwananchi awe na mawasiliano ya uhakika, anayelima kule Sumbawanga awe na mawasiliano ya masoko ya haraka mfano Kariakoo. "
Amesema, mfuko huo katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita unatekeleza miradi 15 ikiwemo ujenzi wa minara,ambao ni mradi wa kimkakati.
"Kwenye Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, sisi (UCSAF) tunaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa minara 758."
Amesema, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kukamilika kwa mradi huo unatarajiwa kunufaisha wananchi zaidi ya milioni 8.5 nchini.
Mhandisi huyo amesema kuwa, Mei 2023, Serikali kupitia UCSAF iliingia mikataba na watoa huduma kufikisha mawasiliano maeneo ya vijijini ambapo kupitia mradi huo kata 713 zitanufaika ambapo minara hiyo itajengwa.
"Pia, halmashauri za wilaya 127 ndani ya mikoa 26 itanufaika ambapo wananchi milioni 8.5 watafikiwa na huduma za uhakika za mawasiliano."
Amesema, kupitia mradi huo Serikali imetoa ruzuku ya shilingi bilioni 126 ili kuufanikisha.
Mradi mwingine wanaotekeleza ni ufungaji wa huduma za intaneti ya bure katika maeneo ya wazi ambapo hadi sasa wamefunga katika vituo saba nchini na maeneo 17 katika viwanja vya Maonesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Pia,amesema mfuko unaendelea kuwajengea walimu uwezo ili waweze kwenda kuwafundisha kwa ufanisi wanafunzi kuhusu Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Amesema, tayari walimu 3,798 wamepatiwa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka shule 1,791 za sekondari nchini.
"Lengo la mafunzo ni kuwajengea uwezo walimu na kutatua matatizo ya vifaa TEHAMA, tayari walimu 3,798 wamepata mafunzo hayo katika shule 1,791.
"Kwa Zanzibar walimu ni 326 na Tanzania Bara walimu ni 3,180 na mafunzo hutolewa pale DIT, UDOM na MUST.
"Katika kipindi cha miaka minne ya Awamu ya Sita walimu 1,585 wamepata mafunzo ya TEHAMA."
Mhandisi Mwasalyanda amesema,pia mfuko umeanzisha utaratibu wa kuwachukua wanafunzi wa kike wakati wa likizo na kuwajengea uwezo kuhusu TEHAMA katika maeneo maalum.
Amesema,lengo ni kupata wabunifu wengi wa kike na kuongeza wataalamu wa TEHAMA nchini. Kupitia mradi huo,wanafunzi 490+248 kutoka shule zaidi ya 300 nchini wamenufaika.
Pia, amesema kuna mradi mwingine wa kupeleka vifaa vya TEHAMA katika shule za wenye mahitaji maalum. Kwa sasa, shule 22 zimeshanufaika kupitia mradi huo ambao umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.8 nchini.
Amesema,Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ulianzishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Sheria ya Bunge nambari 11 ya mwaka 2006 Sura ya 422 kwa lengo la kupeleka na kufanikisha huduma ya mawasiliano kwa wananchi waishio katika maeneo machache ya mijini.
Sambamba na maeneo mengi yaliyo mbali vijijini yasio na mvuto wa kibiashara kwa watoa huduma ya mawasiliano.
Vilevile,mwaka 2009 kanuni za kuhuisha mfuko zilipitishwa na Mfuko kuanza kazi Julai Mosi, 2009.
Tags
Habari
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Kikao Kazi Msajili wa Hazina
Ofisi ya Msajili wa Hazina
UCSAF Tanzania
