TABORA-Wakulima wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora wameanza kunufaika kwa kiasi kikubwa na elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwenye zao la pamba, elimu iliyotolewa kwa ushirikiano baina ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na Bodi ya Pamba Tanzania (TCB).
Wataalamu wa kilimo kutoka TFRA, Bodi ya Pamba, Afisa Ugani na wakulima wa Kata ya Mbutu Wilaya ya Igunga wakipiga hesabu na kubaini uzalishaji wa pamba katika shamba la Tigana Lazaro lenye ukubwa wa ekari moja ni kuzalisha kilo 1,600 tofauti na uzalishaji wa kilo 200 alipokuwa hatumii mbolea ikiwa ni ongezeko mara dufu.Wakulima wakiendelea na zoezi la kuvuna pamba katika shamba la Simon Lukala wa kijiji kijiji cha Mbutu Madukani Kata ya Mbutu Wilaya ya Igunga aliyenufaika na elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwenye zao la pamba iliyotolewa msimu wa kilimo 2024/2025 na kubaini tija.
Wakizungumza wakati wa kufanya tathmini ya uzalishaji baada ya kutumia mbolea, wakulima hao wamesema wanatarajia kuvuna zaidi ya mara tatu ya walichokuwa wakivuna kabla ya kutumia mbolea.
Aidha, wakulima hao wamesema, baada kupata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea ambayo iliambatana na ushauri wa kupima afya ya udongo wamechukua hatua za makusudi kwa kupima na kutambua aina na kiasi cha virutubisho kinachohitajika kwenye mashamba yao na hivyo kutumia mbolea kwa usahihi.
Mtaalam wa Kilimo kutoka Bodi ya Pamba Daniel Bariyanka akimuhoji mkulima wa zao la pamba wa kata ya Mbutu wilayani Igunga, Tigana Kulwa Lazaro (wa tatu kutoka kushoto) hatua alizopitia kupanda na kuweka mbolea kwenye shamba lake mpaka wakati wa mavuno ili kukamilisha tathmini ya manufaa yaliyotokana na uzingativu wa kanuni bora za kilimo walizofundishwa msimu wa kilimo 2024/2025.Kufuatia manufaa waliyoyaona msimu huu, wakulima wa pamba wameahidi kuendelea kutumia mbolea kwenye kilimo ili kuendelea kunufaika na tija inayotokana na matumizi sahihi ya mbolea.
Akishuhudia hayo mkulima, Lucas Sita aliyetenga nusu ya shamba lake na kutumia mbolea na nusu kapanda bila mbolea anaeleza kuwa, shamba alilotumia mbolea limestawi vizuri na kuwavutia wakulima wenzake ambao hawakusita kumtembelea ili kujifunza mbinu alizotumia na kupelekea kuongeza uzalishaji.
Lucas anaeleza kuwa, kabla ya kutumia mbolea kwenye kilimo chake alikuwa akivuna kilo 200 kwa ekari, lakini msimu huu anatarajia kuvuna zaidi ya kilo 1,700 kutokana na tathmini iliyofanywa na wataalamu.
Mtaalam wa Kilimo kutoka Bodi ya Pamba, Daniel Bariyanka akihesabu vitumba vya pamba na kubaini eneo lililolimwa kwa kutumia mbolea ina vitumba 23 na vitumba 10 eneo lililopandwa pasi kutumia mbolea."Kwa kweli nimeonja faida ya kutumia mbolea, siwezi kuacha kuitumia" Lucas alisisitiza.
Naye, Afisa Ugani wa kijiji cha Mwabakima Kata Mbutu wilayani Igunga, Regan Kimario amesema, wakulima wa Kata hiyo wamenufaika na elimu ya mbolea na kilimo cha kuzingatia kanuni bora za kilimo ambayo imeongeza uzalishaji kutoka chini ya kg 500 hadi kufikia zaidi ya kilo 1,000 za pamba kutegemeana na namna mkulima anavyohudumia shamba lake na hali ya hewa.
Tags
Bodi ya Pamba
Habari
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania
Sekta ya Kilimo Tanzania
TFRA Tanzania
