Wakulima wa parachichi wapongeza ruzuku ya Mbolea,wapendekeza utafiti mbolea maalum ya zao hilo

NJOMBE-Wakulima wa parachichi mkoani Njombe wameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia mbolea ya ruzuku ambayo imewasaidia kuongeza tija na uzalishaji katika zao hilo.
Wakizungumza na wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) walipotembelea Chama cha Msingi cha Ng’anda AMCOS na kampuni ya mkulima wa parachichi ya Avo Nemes Green Limited, tarehe 28 Mei, 2025, wakulima hao walisema ruzuku hiyo imepunguza gharama za uzalishaji na kuwawezesha kuajiri nguvu kazi zaidi kwenye mashamba yao.

Mkulima mkubwa wa parachichi, Bw. Stephen Mlimbila, alieleza kuwa kupitia ruzuku hiyo, amepunguza gharama na fedha alizokuwa akizitumia kununua mbolea sasa zimeelekezwa kwenye ulipaji wa vibarua wanaohudumia shamba lake lenye ukubwa wa ekari 210 na kuwa chanzo cha ajira kwa wananchi wengi wasiokuwa na kazi.
Akijibu ombi la wakulima wa chama cha Ushirika Ng’anda cha kusajiliwa kuwa wakala wa mbolea za ruzuku, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, John Cheyo, amemwelekeza Meneja wa TFRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bw. Joshua Ng’ondya, kuhakikisha Chama hicho kinasajiliwa na kusaidia kusambaza pembejeo hiyo kwa wanachama wake na kutatua changamoto ya ucheleweshaji pindi inapohitajika.

Cheyo alisisitiza kuwa serikali inatamani kuona wakulima wanaongeza tija na uzalishaji, akiwahimiza kulima kwa bidii ili kuzalisha mara mbili zaidi ya msimu uliopita ili kukuza uchumi wao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya GBRI Business Solutions Company Limited, inayojihusisha na ununuzi na uongezaji thamani wa zao la parachichi Hadija Jabir, amewasihi wakulima kuzingatia matumizi sahihi ya mbolea kwenye zao la parachichi ili wazalishe kwa wingi na ubora unaohitajika kwenye soko la nje.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news