Wanafunzi Kasulu watakiwa kushiriki UMITASHUMTA

Na Respice Swetu, Kasulu

Walimu wa shule za msingi mkoani Kigoma, wametakiwa kuwaruhusu wanafunzi wa shule zao kushiriki katika mashindano ya umoja wa michezo na taaluma kwa shule za msingi Tanzania UMITASHUMTA yanayofanyika kila mwaka.
Wito huo umetolewa na afisaelimu taaluma wa mkoa wa Kigoma Shukrani Kalegamye wakati wa kikao cha tathmini ya mtihani wa upimaji wa darasa la saba kilichofanyika kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya Bogwe mjini Kasulu.

Akizungumza katika kikao hicho kilichowakutanisha maafisaelimu wa halmashauri, wathibiti ubora wa shule, maafisaelimu wa kata na walimu wakuu wa mkoa huo Kalegamye amesema, kuna uhusiano mkubwa kwa mtoto kufanya vizuri katika michezo na kufanya vizuri katika taaluma.

Kuthibitisha kauli hiyo, Kalegamye ametolea mfano wa halmashauri ya wilaya ya Kakonko iliyofanya vizuri kwenye mtihani wa upimaji wa darasa la saba mkoa wa Kigoma uliofanyika mwezi Mei mwaka huu na kwenye mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya mkoa.
‘’Kuna baadhi ya walimu na wazazi wanawazuwia watoto wao wa darasa la saba kushiriki mashindano ya UMITASHUMTA kwa kisingizio cha kujiandaa na mtihani, nawahakikishia kuwa watoto wanaoshiriki michezo kikamilifu huwa hawafeli, michezo huchamgamsha akili na ndio maana wanaporudi husoma kwa bidii, huelewa haraka na kufanya vizuri pengine zaidi hata ya waliobaki”, amesema.

Ameongeza pia kuwa kupitia mashindano hayo, wanafunzi wanaofanya vizuri kitaifa huchaguliwa kujiunga katika vituo vya kukuza vipaji na kupata fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na ufadhili wa masomo.

Baadhi ya washiriki wa kikao hicho walifika katika chuo cha ualimu Kasulu yalipokuwa yakifanyika mashindano ya UMITASHUMTA na kuishuhudia halmashauri ya wilaya ya Kakonko ikiibuka kidedea kwa kuwa washindi wa jumla huku kikundi cha kwaya cha halmashauri hiyo, kikijikatia tiketi ya kuuwakilisha mkoa wa Kigoma kwenye mashindano ya kitaifa yaliyopangwa kufanyika mkoani Iringa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news