AfIGF 2025 waacha alama Tanzania, wakubaliana mambo mazito

NA GODFREY NNKO

MKUTANO wa 14 wa Jukwaa la Utawala wa Mtandao barani Afrika (AfIGF) 2025 ambao ulianza Mei 29,2025 umetamatika Mei 31,2025 jijini Dar es Salaam huku washiriki ambao ni wawakilishi wa mataifa ya Afrika na wadau mbalimbali wakiwemo watunga sera, wabunge, sekta binafsi, wataalamu, vijana wanaharakati, mashirika ya kiraia na taasisi za elimu ya juu wakiazimia na kutoa mapendekezo mbalimbali.
Jukwaa hilo la siku tatu limefanyika katika kumbi za mikutano za Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam ambapo lilifunguliwa Mei 30,2025 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Mheshimiwa Jerry William Silaa (Mb) kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dotto Biteko.

Aidha, mkutano wa jukwaa hilo umefungwa Mei 31,2025 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla likiongozwa na kaulimbiu isemayo 'Kuwezesha Mustakabali wa Kidijitali wa Afrika'.
Washiriki wa jukwaa hilo kwa umoja wao wamesema,wanathamini Mkataba wa Kuasisiwa kwa Umoja wa Afrika na malengo ya Ajenda 2063.

Hivyo,wanatambua mfumo wa msingi unaojumuisha Mkataba wa Malabo kuhusu Usalama wa Mtandao na Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Vilevile,Mkakati wa Umoja wa Afrika kuhusu Akili Unde (AI), Mkakati wa Afrika wa Mabadiliko ya Kidijitali na Tamko la Afrika kuhusu Kanuni za Uhuru wa Kujieleza na Upatikanaji wa Taarifa.
Kupitia maazimio yao, kwa pamoja wamesema vyombo hivyo vinaakisi maono ya Afrika yenye mafanikio iliyoungana na yenye uwezo wa kidijitali, ikiongozwa na raia wake na kuwa nguvu ya mabadiliko katika nyanja za kimataifa.

Pia,wamesema wanakumbuka ahadi zilizotolewa kwenye Mkutano wa Dunia kuhusu Jamii ya Habari (WSIS) uliofanyika jijini Geneva nchini Uswisi mwaka 2003 na Tunis nchini Tunisia mwaka 2005 hususani kuhusu kupitishwa kwa tamko la kanuni na tafsiri za kazi za utawala wa mtandao.
Katika hatua nyingine, washiriki hao kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika wameangazia Vipengele vya Ajenda ya Tunis aya ya 72 hadi 73 kuhusu kuanzishwa kwa Jukwaa la Utawala wa Mtandao (IGF) lenye mamlaka ya kujadili masuala ya sera ya umma yanayohusiana na vipengele muhimu vya utawala wa mtandao.

Ni kwa lengo la kuimarisha uimara, usalama, uthabiti na maendeleo ya mtandao ikiwa miongoni mwa malengo mengine.

Aidha,wamesema wanatambua IGF kama mojawapo ya mafanikio makubwa ya mchakato wa WSIS na wamethibitisha nafasi yake muhimu kama jukwaa la wadau mbalimbali kwa ajili ya majadiliano juu ya sera zinazohusiana na mtandao.

Washiriki hao, wamesema pia wanatambua mchango wa uongozi wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi kwa Afrika (UNECA) kwa kushirikiana na Tume ya Umoja wa Afrika, sekta binafsi na mashirika ya kiraia, katika kukuza ushiriki wa Afrika kwenye mchakato wa utawala wa mtandao na sera za kidijitali duniani ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa AfIGF.

Mbali na hayo,wamekaribisha kupitishwa kwa Mkataba wa Kidijitali wa Dunia (GDC) kama kiambatanisho cha mkataba kwa ajili ya baadaye huku wakithibitisha umuhimu wake katika kusukuma mbele gurudumu la mabadiliko ya kidijitali yenye usawa, salama na jumuishi.
Sambamba na mafanikio ya WSIS na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Pia,washiriki hao kwa pamoja wametoa tamko kuwa,wanatambua kuwa Mkataba wa Kidijitali wa Afrika (ADC) unaoendana na GDC umejikita katika kujenga Afrika yenye uwezo wa kidijitali ambapo teknolojia inachochea ukuaji wa uchumi, ustawi wa kijamii na mustakabali wenye mafanikio kwa wote.

Jambo lingine wamesema,wanatambua zaidi kuwa Tamko la Umoja wa Afrika kuhusu Utawala wa Mtandao linaimarisha maono ya pamoja ya Bara la Afrika kwa ajili ya mustakabali wa kidijitali ulio huru, jumuishi, unaozingatia haki na unaoelekezwa katika maendeleo.Washiriki hao, pia hawakusita kusema kuwa, wanakumbuka Tamko la Cotonou kuhusu Afrika WSIS+20 kama msingi wa kueleza msimamo wa pamoja wa Afrika kuhusu utawala wa kidijitali, uchumi wa kidijitali na maendeleo jumuishi.

Pia,wamesema mamlaka ya IGF yatapitiwa upya na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwezi Desemba,2025, hivyo wanathibitisha tena uungaji mkono thabiti kwa kuendelea kwake na kuimarishwa kwa taasisi hiyo.
Wakati huo huo, washiriki wa AfIGF 2025 wametangaza kwa pamoja dhamira yao ya kuimarisha mustakabali wa kidijitali wa Afrika kupitia utawala wa mtandao wa kidemokrasia, unaozingatia haki na kushirikisha wadau mbalimbali.

Wamesema ili kufanikisha hilo,wanajitolea kuandaa mpango kazi madhubuti unaoshughulikia changamoto kuu na kufungua fursa kwa ajili ya ukuaji endelevu wa kidijitali.

Katika hatua nyingine, wamesema wanatambua mafanikio yaliyopatikana kupitia mchakato wa WSIS huku pia,wakitambua changamoto zinazoendelea kuzuia ushiriki kamili wa Afrika katika uchumi wa kidijitali wa Dunia.
Aidha, jukwaa hilo la kwanza kufanyika hapa nchini limewezesha kujenga ushirikiano wa pamoja katika kuunda sera na mifumo ya kidijitali inayohudumia maslahi ya wote barani Afrika kwa ustawi bora wa huduma za intaneti.
Katika jukwaa hili wataalamu wa masuala ya mtandao barani Afrika wamejadili kwa kina mada mbalimbali ikiwemo Akili Unde (AI) na teknolojia zinazoibuka,miundombinu ya umma ya kidijitali na usimamizi wa taarifa.

Changamoto

Kupitia majadiliano yao,washiriki hao walibainisha changamoto mbalimbali ikiwemo upande wa miundombinu na uunganishaji wa mtandao.

Wamesema,sehemu kubwa ya watu barani Afrika bado wameachwa nyuma kutokana na ukosefu wa mtandao mpana wa intaneti, gharama kubwa za data na upatikanaji mdogo wa njia fanisi za upitishaji mawasiliano kwa kasi.

Vilevile, wamesema kuna changamoto upande wa usimamizi wa rasilimali za mtandao huku wakibainisha kuwa,Kituo cha Taarifa cha Mtandao cha Afrika (AFRINIC) kinakumbwa na changamoto kubwa za kiutendaji na kiutawala.

Hali hiyo inachagizwa na kutokuwepo kwa uthabiti wa kifedha,migogoro ya uongozi na ukosefu wa uhakika wa kisheria,hali inayotishia usimamizi bora wa rasilimali za mtandao.
Changamoto nyingine wamesema kuwa ni upande wa ujumuishaji wa kidijitali,kwani makundi yaliyo katika mazingira magumu na pembezoni yakiwemo watu wenye ulemavu, wakimbizi na watu wasio na utaifa, wanawake, vijana wa vijijini na wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi, bado wanakosa fursa za kidijitali.

Kukosekana kwa utayari wa kisheria na kiusimamizi, wamesema sera za kidijitali na mifumo ya udhibiti isiyoratibiwa kati ya nchi wanachama inazuia uundaji wa mazingira ya kidijitali yaliyo thabiti, yanayozingatia haki na yanayochochea ubunifu.

Aidha,wamesema mifumo ya elimu haina ujumuishaji wa maarifa ya juu ya kidijitali kama vile akili unde (AI), taarifa kubwa na usalama wa mtandao.

Wamesema,pia mitaala mingi ya shule haijajumuisha elimu ya TEHAMA katika ngazi ya msingi, jambo linalozuia watoto kupata ujuzi wa kidijitali mapema.
Changamoto nyingine wamesema ni uwepo wa mifumo dhaifu ya ulinzi wa taarifa na uwezo mdogo wa kiusalama mtandaoni unaziweka nchi hatarini kwa uhalifu wa kimtandao, uvunjaji wa faragha ya taarifa na mashambulizi kwa miundombinu muhimu.

Changamoto nyingine wamesema,kuna mapungufu katika mifumo ya kufafanua majukumu, uwajibikaji na taratibu za usimamizi kati ya wadau muhimu, pamoja na ukosefu wa mifumo madhubuti ya kuwasilisha na kutetea misimamo ya pamoja ya Afrika kuhusu masuala ya utawala wa mtandao.
Aidha,wamesema kuna upungufu wa maudhui ya kidijitali yaliyo katika lugha za asili na yanayozingatia muktadha wa kitamaduni ambapo unadhoofisha ujumuishaji wa kidijitali na uhifadhi wa urithi wa kitamaduni.

Changamoto nyingine wamesema, ni upatikanaji usiotabirika wa umeme unaendelea kuathiri uwekezaji na upanuzi wa TEHAMA pamoja na uunganishaji wa mtandao maeneo mengi kwa nchi za Afrika.

Utekelezaji

Kwa pamoja,washiriki hao wamekubali kuanzisha mfumo wa Bara la Afrika wa kufuatilia na kutathmini maendeleo, wenye ripoti kila baada ya miaka miwili kwa Afrika IGF ili kuhakikisha uwazi na maamuzi yanayotegemea ushahidi kamili.
Pia,wamekubali kuondoa pengo la kijinsia katika matumizi ya teknolojia, kukuza uongozi wa wanawake katika utawala wa mtandao na kuwawezesha vijana wa Afrika kushiriki katika uundaji wa sera na suluhisho za kidijitali.

Jambo lingine wamekubali kuwezesha, kukuza na kuendeleza huduma za kidijitali kwa lugha za asili za Kiafrika na kuhifadhi maarifa ya jadi kupitia majukwaa jumuishi ya kidijitali.

Aidha,wamekubali kujumuisha uendelevu wa kimazingira na mabadiliko ya kidijitali yanayozingatia hali ya hewa.

Ni kwa kupitisha sera za TEHAMA rafiki kwa mazingira, kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali isiyo na kaboni nyingi na kukuza uchumi wa mzunguko ikiwemo usimamizi wa taka za kielektroniki.

Pia,wamekubali kuwahimiza washirika wa kimataifa kusaidia mabadiliko ya kidijitali yanayoongozwa na Afrika kupitia uwekezaji, msaada wa kiufundi na ushiriki wa haki katika michakato ya utawala wa kimataifa.
Washiriki hao pia, wamekubali kulinda haki za binadamu na uhuru wa kidijitali ikiwa ni kwa kuheshimu haki za msingi ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza, upatikanaji wa taarifa, faragha na ulinzi dhidi ya ubaguzi katika sera na teknolojia zote za kidijitali.

Vilevile,kusaidia maendeleo na uendelevu wa Mabaraza ya Kitaifa na Kikanda ya Utawala wa Mtandao (NRIs) kama majukwaa jumuishi yanayolingana na mchakato wa Afrika IGF.

Washiriki,pia wamekubali kuimarisha uratibu wa ndani ya Afrika ili kuhakikisha ushiriki madhubuti na endelevu wa barani humo katika mabaraza ya kimataifa ya utawala wa mtandao na mengineyo.
Wakati akifunga mkutano huo,Katibu Mkuu,Mohammed Khamis Abdulla amesema, wamekubaliana kuwezesha jamii za chini hasa vijijini waweze kutumia huduma za mawasiliano.

Pia, amesema Serikali ya Tanzania imewafungulia milango ili kuja muda wowote kujifunza namna tulivyofanya, tumefika wapi na wao wakafanye nini ili kuimarisha huduma za mawasiliano.

Amesema, katika jukwaa hilo lilijikita zaidi katika majadiliano ambayo yaliwahusisha wataalamu kutoka Tanzania, ndani ya Afrika na duniani.
Pia, amesema Tanzania imechahuliwa kuendesha kongamano hilo kutokana kuwa nchi ya mfano barani Afrika kwenye mambo ya mitandao.

"Imeonekana kwamba Tanzania ni nchi ambayo tumeweza kuyafikia maeneo mengi, kuwajumuisha wananchi kote nchini ikiwemo vijiji kwa kuwafikishia mawasiliano ili kufanya huduma mbalimbali za Serikali.

"Kwa hiyo, AfIGF Afrika ikaona ni vema twende Tanzania, tukafanye hili jukwaa na pia kuja kwao hapa ni ili waweze kujifunza sisi kama Tanzania tumewezaje.Kwa sababu limekuwa ni jambo la changamoto kubwa sana kwenye nchi nyingine za kiafrika.
"Kwa hiyo, tumekuwa na hili jukwaa leo ni siku ya mwisho, tumefunga na tumekuja na maazimio ambapo maazimio hayo tutaenda nayo kwenye AfIGF ya Dunia.Leo, tumemaliza AfIGF ya Afrika ."

Amesema, wamejadiliana mambo mengi na kuazimia kama Afrika watakapoenda katika AfIGF ya Dunia watakutana na nchi mbalimbali duniani, hivyo kama Afrika watakuwa kitu kimoja, hivyo ili waweze kwenda na kasi ya Sayansi na Teknolojia wataainisha mambo ambayo wanataka kuyafanya.
"Mambo hayo ni yale ambayo leo tumekubaliana, kwa hiyo kikao kimeenda vizuri na tumekubaliana mambo yote ya utekelezaji tumekubaliana tuwezeshe jamii zetu za chini hasa vijijini waweze kutumia huduma za mawasiliano."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news