DAR-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema madhehebu ya dini yana mchango mkubwa katika kuimarisha ustawi wa jamii na kutoa huduma za kiroho.

Amesema hayo leo Mei 10, 2025 alipomuwakilisha Mheshimiwa Dkt. Samia katika kilele cha dua maalum ya kuombea viongozi wa Kitaifa, amani, uchaguzi mkuu pamoja na kuwaombea mamufti na masheikh waliotangulia mbele za haki, kwenye Viwanja vya Msikiti wa Mohammed VI, Kinondoni Dar es Salaam.

Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amempongeza Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir bin Ali Mbwana kwa kuandaa dua hiyo kwa ajili ya baraka na amani ya Tanzania wakati wa uchaguzi mkuu.
“Nikiri kwamba Serikali inatambua umuhimu wa sala na dua. Viongozi tunatekeleza majukumu yetu kwa salama kwa kuwa viongozi wetu wa dini na waumini wote mnatuombea dua. Hii ndiyo sababu Serikali imekuwa ikishirikiana na madhehebu ya dini katika shughuli zake.”
Ameongeza kuwa Serikali inathamini kazi kubwa inayofanywa katika maeneo mbalimbali hususan katika kutoa huduma za kijamii na hivyo kuchangia kasi ya maendeleo ya Taifa letu. “Huduma hizo ni pamoja na zile za elimu, afya, maji, nishati, mafunzo kuhusu kilimo bora na ufugaji, na huduma nyingine mbalimbali.”
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya dua hiyo Kitaifa Hajati Mwamtumu Mahiza amesema kuwa dua hiyo ni kwa ajili ya kuwaombea masheikh na Mamufti walioleta mchango chanya katika dini ya kiislamu.

“Tunahitaji kuwa wanyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu anasema katika Quran kuwa niombeni nami nitawapa, tunataka kuingia kwenye uchaguzi mkuu na kutoka tukiwa salama na wamoja.”